WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba mjini kuaaga miili ya watu 16 waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea jana (Jumamosi, 10 Septemba, 2016 mkoani Kagera.
 
Tetemeko hilo lilitokea jana Alasiri limesababisha vifo vya watu 16 na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.
 
Kufuatia tukio hilo Waziri Mkuu ambaye alimuwakilisha Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya athari zilizotokana na maafa hayo.
 
“Poleni sana tukio hili ni kubwa na halijawahi kutokea nchini. Haya yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Tuendelee kuwa na imani na watulivu  Serikali ipo pamoja nanyi na haitawatupa mkono,” amesema.
 
Waziri Mkuu amesema Kamati ya Maafa ambayo ipo katika Ofisi ya Waziri ya Mkuu itakwenda wilaya za Kyerwa, Karagwe na Bukoba mjini kwa ajili ya kufanya tathmini na kubaini athari zilizosababishwa na tetemeko hilo na kuona namna ya kuwasaidia waathirika.
 
Wakati huo huo Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa mkoa huo kuchukua hatua za haraka kwa kuwatafutia eneo salama la kulala wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyakato ambayo mabweni yake yote yameathirika na tetemeko hilo na hayafai kutumika.
 
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea namna mabweni ya shule hiyo yalivyopata nyufa hali iliyosababisha wanafunzi kulala uwanjani.
 
Pia Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuangalia kama kuna tetemeko linguine linaweza kutokea nchini ili Serikali iweze kuchukua tahadhari pamoja na kutoa elimu kwa umma namna ya kujikinga.
 
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu amesema kwa sasa wanaendelea na jukumu la kuwatafutia makazi wananchi ambao nyumba zao zimeanguka. Pia mkoa unaendelea kufanya tathmini ya kina kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.
 
Awali Waziri Mkuu alitembelea Hospitali ya Mkoa wa Kagera ambako majeruhi 170 wamelazwa na kutoa pole na kwamba anawaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na wenye matatizo ambayo yanahitaji matibabu kwenye hoispitali kubwa Serikali itahakikisha wanapelekwa huko na kuhudumiwa.
 
(mwisho)
 IMETOLEWA NA:              
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI,SEPTEMBA 11, 2016

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...