Waziri MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia sasa mtu yeyote mwenye shida ya kuonana naye itabidi amfuate Dodoma na kwamba atarudi Dar es Salaam pindi akiitwa na Mheshimiwa Rais au Makamu wa Rais.


Ametoa kauli hiyo leo jioni (Ijumaa, Septemba 30, 2016) wakati akizungumza na viongozi mbalimbali na wakazi wa mji wa Dodoma waliofika kumpokea mara baada ya kuwasili mjini hapa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa Julai 25 kuwa atahamia Dodoma ifikapo Septemba mwaka huu.


“Tukio hili la kuhamia Dodoma si la mzaha, hakuna siasa na wala si jaribio. Tumeshakeleza. Kama kuna waliokuwa wanafiria kwamba halitekelezeki watambua kwamba tayari tumeshafika. Na kuanzia sasa atakayetaka huduma ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu amesema Dodoma si ndogo kama baadhi ya watu wanavyodai na kwamba  huduma zilizopo zinatosha kukidhi mahitaji ya sasa. "Mkakati uliopo wa kupanua huduma za tiba, maji, umeme na masoko utawezesha watumishi wote kuishi bila bugudha yoyote."


“Awamu ya kwanza inaanzia Septemba hadi Februari mwakani. Mimi nimeshatangulia na wanaofuata ni mawaziri na manaibu wao wote, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wote. Natambua kwamba wote wana nyumba za kuishi na kama wapo ambao hawana hawazidi asilimia tano na nyumba zipo


Amewataka watumishi wote wa Serikali watambue kwamba safari imeshaanza na kila mmoja ajipange, na akarudia wito wa Mheshimiwa Rais kwamba atakayegoma kuhamia Dodoma atakuwa amejifukuza kazi.

Waziri Mkuu amewataka watendaji wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) wasifanye kazi kwa mazoea, bali wabadilike na kwa kuwa amehamia Dodoma ameahidi kuafuatilia kwa karibu zaidi.

Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi (OWM SUBKAV), Jenista Mhagama amesema kilichofanyika leo ni uthibitisho kuwa yale ambayo Serikali ya Awamu ya Tano iliahidi sasa hivi imeanza kuyatekeleza.


"Tuliahidi kukusanya kodi, tuliahidi elimu bure, tuliahidi kupambana na mafisadi, tuliahidi kuondoa watumishi hewa, tuliahidi kuifufua ATCL na kununua ndege mpya na yote tumetekeleza,” amesema.


Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. George Simbachawene amesema uamuzi wa kuhamia Dodoma ni uthibitisho kuwa  viongozi wetu kweli wamedhamiria kutekeleza ahadi ya Baba wa Taifa ya kuhamishia makao makuu ya nchi hapa Dodoma.


"Dodoma imeanza kuchangamka na hii ni fursa tosha kwa mkoa wetu kubadilika. Tushirikiane na CDA kuijenga Dodoma mpya. Kitendo cha Mheshimiwa Waziri Mkuu kuingia Dodoma leo hii maana yake ni kwamba Serikali iko rasmi Dodoma," amesema.


Hafla hiyo ilihudhuriwa na Manaibu Waziri Anthony Mavunde na Dk. Ashatu Kijaji, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Rais (Utumishi), Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo, wazee wa mkoa huo, viongozi wa dini, viongozi wa taasisi zilizoko mkoani na baadhi ya wananchi.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA

IJUMAA, SEPTEMBA 30, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakiwapungia akiwapungia wananchi wa Dodoma baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Septemba 30, 2016.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha ufunguo aliokabidhiwa na Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jafar Mwanyemba (kushoto) kuashiria kupokewa rasmi kwenye manispaa hiyo. Makbidhiano hayo yalifanyika kwenye makazi yake eneo la Mlimwa Septemba 30, 2016.
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa na mkewe Mary wakiagana na watuimishi wa Makazi ya Waziri Mkuu ya Dar es salaam kabla ya kuondoka kuelekea Dodoma Septemba 30, 2016 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakisalimiana na Madiwani wa Manispaa ya Dodoma baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma Septemba 30, 2016.
Waziri Mkuu, Kasim Majliwa akiwapungia wananchi baada ya kuwasili kwenye makazi yake mjini Dodoma Septemba 30, 2016.  

PICHA ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...