Mzee Philip Mangula
Na Bashir Nkoromo, Mkuranga
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula ameelezea kufurahishwa kwake kufukuzwa kwa wanachama 100 mkoani Mwanza kwa kubainika kukisaliti chama wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

"Haiwezekani, unajiita mwanachama, halafu badala ya kujitolea kwa nguvu zako zote chama kishinde vita ya kushika dola, wewe unakisaliti,  hapo unakuwa si mwanachama bali jeshi la kukodiwa",  Mangula alisema, hayo jana, wakati akizungumza na Vijana wanaosoma na waliohitimu vyuo vikuu 20, ambao wameweka kambi ya kufyatua matofali kwa ajli ya ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu katika shule ya Sekondari Nasabagani, Mkuranga mkoa wa Pwani.

 "Taarifa ya Chama kuwafukuza uanachama wale 100 kule Mwanza imenifurahisha sana, ni matumaini yangu kwamba hatua kama hizi zitaendelea kuchukuliwa  kila mahala nchini kote kwa waliokisaliti chama. hivi ni mchezaji gani anayempiga ngwara mchezaji wa timu yake wakati wa mechi ya kutafuta ubingwa halafu akaachwa kuendelea kuwa katika timu?" Mangula alisema na kuhoji kwa mshangao.

Mangua alisema, wakati mikoa itaendelea kuchukua hatua, lakini pia kwa ngazi ya taifa hatua dhidi ya waliokisaliti chama zitaendelea kuchukuliwa, ikiwa ni pamoja na kuwatupilia mbali watakaojaribu kuomba nafasi za uongozi wakati wa uchaguzi wa Chama mwakani, huku wakiwa wameshabainika kuwa walikisaliti chama wakati wa uchaguzi mkuu ulipita.

Mangula aliwataka vijana nchini kote hasa wasomi, kuepuka kutumiwa vibaya na wanachama watakaokuwa wanasaka uongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwakani, kwa kuwa kijana yeyote atakayekubali kutumiwa vibaya atakuwa amekisaliti na kuchangia kunyong'onyesha nguvu na uhai wa Chama.

"Hili la kutumiwa vibaya hasa ninyi vijana, nawaasa sana kuepuka nalo, jambo hili ni baya sana, na si kwa Chama tu lakini hata kwa wewe uliyekubali kutumika, maana utatumiwa kama ngazi, halafu akishapita hatakuwa na manufaa kwako na hata kwa taifa maana atakuwa mvurugaji tu, badala ya kushiriki kuleta maendeleo ya chama na taifa", Alisisitiza mangula.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...