Na Ally Daud-MAELEZO.

MUSWADA wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 umeonekana kuwa mlinzi kwa wanahabari nchini kwa kuwa na kipengele kinachowataka waajiri kuwapa bima na mifuko ya hifadhi ya jamii waajiriwa wake mara baada ya kuwaajiri kama wafanyakazi halali wa chombo husika.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti na Mratibu wa kampeni ya Media Car Wash for Cancer Bw. Benjamin Thomson Kasenyenda wakati wa kutoa maoni kuhusu Muswada wa Sheria ya huduma za Habari ya 2016 hivi karibuni.

“Hakika Muswada huu umekuja muda muafaka kwani tumepitia changamoto nyingi sana kama wanahabari ikiwa ni kupata ajali na kuugua mara kwa mara bila ya kuhudumiwa chochote na wamiliki wa vyombo husika vya habari hapa nchini” alisema Bw. Kasenyenda.

Aidha Bw. Kasenyenda ambaye pia ni Mwanahabari mkongwe anayetumikia hii tasnia kwa muda mrefu amesema kuwa wanahabari wanatakiwa kuishukuru Serikali kwa kuleta huu muswada kwani una manufaa na ulinzi kwa wanahabari pindi wanapokuwa maeneo yao ya kazi .

Mbali na hayo Mwanahabri huyo mkongwe nchini amesema kuwa wanahabari wanatakiwa kuusoma vizuri huo muswada na kutumia fursa hii kwa kutoa maoni yao ili upite na kuwa sheria nchini na wasicheze ngoma za wanasiasa ambao wanajinufaisha wao wenyewe bila kujali maslahi ya mwanahabari nchini.

Kwa upande wa Mmiliki wa Blogu ya jamii inayojulikana kwa jina la Fullshangwe Bw. John Bukuku amesema kuwa wanaishukuru Serikali kwa kuleta muswada huu kwani kwa upande wa kipengele cha kuwapa bima waandishi wa habari itawafanya wawe salama Katika kazi zao wakati wowote na sehemu yoyote.

“Naishukuru Serikali kwa kuleta muswada wa sheria ya habari hasa kwenye kipengele cha bima na mfuko wa hifadhi ya jamii kwani utakua ulinzi tosha kwa mwanahabari pindi atakapoumwa au kufariki itakuwa msaada mkubwa kwetu sisi wenyewe” alisema Bw. Bukuku.

Naye Mwandishi wa habari wa gazeti la Majira anayeripotia Tanga Bw. Mashaka amesema kuwa wanahabari wasibweteke katika kutoa maoni kuhusu huu muswada kwani ndio kimbilio la haki zao kutoka kwa waajiri wao ili kufanya kazi zao kwa usalama na amani wawapo sehemu zao za kazi.

“Kwakweli wanahabari umefika muda wetu wa kufanya kazi kwa usalama na haki kama muswada huu utapita kwani utatufanya tupate haki yetu ya msingi Katika kazi zetu hivyo tusibweteke kutoa maoni yetu ili tuupitishe huu muswada kwa maendeleo yetu wenye”alisema Bw. Mashaka.

Muswada wa sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 kifungu cha 58(1) kinasema mwajiri ni lazima amwekee bima na mfuko wa hifadhi ya jamii mwajiriwa wake hivyo wanahabari wanatakiwa kutoa maoni yao kupitia cna@bunge.co.tz.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...