WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda timu ya wataalamu ambao watatoa ushauri
juu ya suala zima la kuhamishia makao makuu Dodoma.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumamosi, Oktoba 1, 2016) wakati akizungumza na watumishi
wa Serikali wa mkoa wa Dodoma, wazee wa mkoa huo, wafanyabiashara pamoja na viongozi
mbalimbali kwenye ukumbi wa mikutano wa Dodoma (Dodoma Convention Centre).
“Tumeunda
timu ya watu 10 ambao ni wataalamu waliobobea kwenye masuala ya ujenzi wa miji
mikuu, hawa wana uzoefu wa kuangalia makao Makuu ya nchi yanafananaje. Watakuja
Dodoma, wapitie master plan na kisha watapita
kwenye maeneo kadhaa ya mji ili waone hali halisi ikoje ndipo watupe maoni yao,”
amesema.
“Tunataka
tusirudie kosa la Jiji la Dar es Salaam la kulazimika kubomoa makazi ya watu
kila inapolazimu kufanya uboreshaji wa miundombinu. Hawa watu watatuambia wapi
tunatakiwa tuweke njia nne au sita za magari, wapi tuweke bustani au wapi
tujenge nyumba za ghorofa moja, mbili, tatu au zaidi,” ameongeza.
Akifafanua
kuhusu miundombinu, Waziri Mkuu amesema timu hiyo pia itatakiwa kutoa ushauri
juu ya wapi ijengwe njia ya malori tu au mahali gani zinahitajika kujengwa barabara
za juu (flyovers) ili kuepusha msongamano katikati ya mji wa Dodoma.
Bila
kutaja majina ya wajumbe wa timu hiyo, Waziri Mkuu amesema timu hiyo
itaongezewa wataalamu kutoka China na Malaysia ambao nchi zao tayari zina
uzoefu wa kuhamisha makao makuu ya nchi zao zaidi ya mara moja.
Alitumia
fursa hiyo kuwaeleza watumishi juu ya uwepo wa Tume ya Kuboresha Maslahi ya Wafanyakazi
ambayo imekuwa ikifanya kazi tangu mwaka jana. “Kuna vikao vimekuwa vinafanyika
tangu mwaka jana baina ya Serikali na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa
lengo la kujadili uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi, na jambo hili
linaendelea vizuri,” amesema.
Kuhusu
madeni ya watumishi wa umma, Waziri Mkuu amewasihi watumishi wawe na imani na Serikali
yao kuhusu madeni hayo na kwamba ikimaliza uhakiki unaofanyika hivi sasa, kila
mwenye stahili zake atalipwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ihakikishe
inakamilisha upimaji wa viwanja 100,000 kama ilivyojipangia ili watumishi hao
pamoja na wananchi waweze kupatiwa viwanja haraka iwezekanavyo.
“Nimearifiwa
kuwa mna mpango wa kupima viwanja 100,000 kwa ajili ya kuwapatia wananchi na
watumishi. Kamilisheni utaratibu huo haraka ili watumishi wapewe viwanja na
waweze kujenga nyumba zao za kuishi,” amesema huku akishangiliwa.
Natambua
kuwa mmekubaliana kuanzisha utaratibu wa kuingiza viwanja kwenye mfumo wa
kompyuta ili kuepuka double allocation.
Harakisheni zoezi hilo ili kama itawezekana, kabla ya Novemba kazi hiyo iwe
tayari na watu wapatiwe viwanja chini ya mfumo huo mpya,” amesisitiza.
Kuhusu
huduma za kijamii kama elimu, umeme, maji na masoko, Waziri Mkuu
amewahakikishia watumishi hao kwamba Serikali imeangalia kila eneo na
kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa ili kuboresha utoaji wa huduma hizo. Amewataka
watumishi hao wabadilike na wawe tayari kuwapokea watumishi wenzao
watakaowasili kwa awamu kuanzia mwezi huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA
JUMAMOSI, OKTOBA
MOSI, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa serikali na Taasisi zake mjini Dodoma Oktoba 1, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya watumishi wa serikali na Taasisi zake wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao mjini Dodoma Oktoba 1, 2016. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...