WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutafuta fedha za mafunzo kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini ili kuziba pengo la wahadhiri waandamizi lililopo hivi sasa lakini pia amevitaka vyuo hivyo viweke utaratibu wa kuachiana nafasi ama kurithishana kazi (succession plan).

Amesema yeye binafsi anatambua upungufu uliopo umesababishwa na masharti ya ajira za mkataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Oktoba 25, 2016) wakati akifunga kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Nkrumah. Kampasi ya Mwalimu J. K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Ninatambua kuwa katika vyuo vya umma kuna upungufu mkubwa wa wahadhiri waandamizi na maprofesa na hivyo kuathiri hali ya utoaji wa taaluma kwa fani za ‘Post-Graduates’. Ninajua kuwa pamoja na sababu nyingine, hali hii inachangiwa pia na masharti ya ajira za mikataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo,” amesema.

“Lakini vyuo vya elimu navyo havina budi kuweka taratibu na mipango endelevu ya kurithishana (kuachiana nafasi) ‘Succession Plan’. Jambo hii ni muhimu sana kwani bila hivyo, wakati wote kutakuwa na pengo kubwa katika utoaji wa taaluma,” amesisitiza.

Amesema Serikali itatoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa mipango hii ya kuwa na watalaamu wa kutosha katika vyuo huku ikiendelea kutekeleza majukumu ya kuwaajiri wanataaluma na wafanyakazi wapya pale wanapohitajika.

Akizungumzia kuhusu maslahi ya watumishi wa vyuo hivyo, kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wote wa umma na hivi sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwa watumishi wa umma ili kubaini watumishi hewa.

“Hadi kufikia tarehe 20 Oktoba, 2016 zoezi linaloendelea hivi sasa, limesaidia kuwabaini watumishi wa umma hewa wapatao 16,500. Baada ya zoezi hilo, tutarudia uhakiki wa madeni yote yaliyowasilishwa Serikalini na kisha tutalipa madeni ya watumishi wote,” amesema.

“Ninafahamu kuwa yapo madai mbalimbali ikiwemo malimbikizo ya mishahara kwa watumishi hususan baada ya kuanza kwa muundo wa pamoja wa wanataaluma wa vyuo vikuu vya umma. Serikali inaendelea na maboresho na kuimarisha maslahi kwa watumishi wote wa umma kupitia bodi ya mishahara na motisha; na mara tutakapokamilisha, tutapanga upya mishahara na motisha kwa watumishi,” amesema.

Akifafanua kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa mikopo. Ametoa wito kwa wanufaika na waombaji wote wa mikopo wahakikishe kuwa wanatoa taarifa zilizo sahihi na za uhakika.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali ilikwishaongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka sh. bilioni 340 mwaka 2015/2016 hadi sh. bilioni 483 kwa mwaka 2016/2017.

Mapema, akielezea utendaji kazi wa chuo hicho katika miaka yote 55, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala amesema chuo hicho kinakabliwa na changamoto ya uhaba wa wanataaluma waandamizi wa fani mbalimbali.

“Chimbuko la changamoto hii ni kusitishwa kwa ajira katika taasisi za umma kwenye miaka ya 1990. Kutoajiriwa kwa wanataaluma chipukizi kwa miaka mingi, kulivuruga utaratibu wa miaka mingi wa kurithishana uzoefu baina ya wanataaluma wanaostaafu na wale ambao wangelichukua nafasi zao,” amesema.

“Hali hii iko kwenye vyuo vikongwe ambako mamia ya wanataaluma wazoefu wanastaafu kwa wakati mmoja na wengi wa wanataaluma walioajiriwa hivi karibuni bado wako masomoni au wangali chipukizi katika taaluma zao na hivyo hawana uwezo wa kutosha kubeba majukumu ya kufundisha katika ngazi za digrii za umahiri na uzamivu,” amesema.

Hata hivyo, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kuwadhamini wahadhiri chipukizi ambao wako sehemu mbalimbali wakipata mafunzo. Pia amemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kujenga hosteli yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,800 na hivyo kutarajiwa kupunguza tatizo la malazi.

Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo alisema wizara hiyo imetenga kiasi cha sh. bilioni 9 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu kwenye chuo hicho zikiwemo maabara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...