Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyarugusu, Juma Edward aliyesaidiwa na Shirika la Plan International kuacha kazi migodini na kurudi shule kuendelea na masomo akilishukuru shirika hilo kwa kuanzisha Mradi wa Uondoaji wa Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto, Mradi huu wa miaka mitatu unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), unaratibiwa na Shirika la Plan International na kutekelezwa katika Wilaya 3 za Mkoa wa Geita.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Geita

Shule ya Msingi Nyarugusu iliyopo mkoani Geita imeanzisha kamati ya kudhibiti utoro wa wanafunzi ikiwa ni njia moja wapo ya kuwazuia kwenda kufanya kazi katika migodi iliyopo mkoani humo.

Maamuzi hayo yametolewa na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Peter Kitagira alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya mchango wa Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na kuratibiwa na Shirika la Plan International. 

Kitagira amesema kuwa wameamua kuchukua maamuzi hayo baada ya kugundua kuwa asilimia kubwa ya watoto wa mkoa huo wanaacha shule na kukimbilia kufanya kazi za migodini kwa ajili ya kujitafutia kipato bila kufahamu madhara ya shughuli hizo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyarugusu. Peter Kitagira akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya uanzishwaji wa Kamati ya utoro katika shule hiyo. Mradi huu wa miaka mitatu unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), unaratibiwa na Shirika la Plan International na kutekelezwa katika Wilaya 3 za Mkoa wa Geita.

“Hali ya utoro inaongezeka kwa kasi na ndio maana tumeamua kuanzisha Kamati ya Kudhibiti Utoro wa wanafunzi, kamati hiyo inafanya mawasiliano ya karibu na wamiliki wa migodi ili kuhakikisha hakuna mtoto chini ya umri wa miaka 18 atakayeajiriwa kwa ajili ya kufanya kazi kwenye maeneo hayo”, alisema Kitagira.

Kitagira ameitaja sababu nyingine inayosababisha kushuka kwa mahudhurio ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kuwa ni hali duni ya maisha inayosababisha wazazi kuwaacha watoto majumbani wakilinda nyumba ili wao wakatafute fedha za kujikimu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati wa Shule hiyo, Philip Edward amesema kuwa ni vigumu sana kuwaelimisha wazazi juu ya athari za watoto kufanya kazi migodini au kuwaacha nyumbani wakilinda nyumba na kulea wadogo zao kwa sababu hawana njia nyingine ya kujipatia kipato zaidi ya kufanya kazi hizo.
Mwenyekiti wa Kamati wa Shule ya Msingi Nyarugusi, Philip Edward akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu umuhimu wa mradi wa Uondoaji wa Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), unaratibiwa na Shirika la Plan International na kutekelezwa katika Wilaya 3 za Mkoa wa Geita.

“Ili kupunguza utoro shuleni hapa, kamati ya shule ilifanya kikao na wazazi ambapo tulikubaliana kutoa kiasi cha shilingi mia tano kama adhabu kwa kila mwanafunzi ambaye hatokuja shuleni lakini muda mwingine tunawahurumia wazazi kwani kipato chao ni cha shida sana”, alisema Edward.

Naye Mwalimu wa shule hiyo, Mathias Kato ambaye pia ni mlezi wa watoto wanaohudumiwa na shirika la Plan International amelishukuru shirika hilo kwa jitihada zao wanazozifanya katika kupinga ajira za watoto migodini kwa sababu umechangia kiasi kikubwa kuongeza mahudhurio ya  wanafunzi shuleni hapo.

Ametoa ushauri kwa Serikali na mashirika mengine kuangalia namna ya kuwasaidia wazazi wenye kipato duni wanaoishi katika maeneo ya migodi kwa sababu ukosefu wa kipato kwa wazazi ndiyo chanzo cha watoto kutoroka shule na kwenda kujitafutia ridhiki migodini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...