Katika jitihada za kuboresha huduma kwa walipakodi na kuzifikisha huduma hizo kwa karibu zaidi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA) Bw. Alphayo Kidata amezindua ofisi mpya ya TRA katika eneo la Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam Tarehe 26 Oktoba 2016 itakayotoa huduma zote za kikodi ikiwemo usajili na uhakiki wa Namba za Utambulisho wa Mlipakodi –TIN, Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani-VAT, Malipo ya Kodi za Magari, Kodi zote za Mapato zikiwemo Kodi za Makampuni, Watu Binafsi, Wafanyakazi (PAYE), Kuendeleza Ufundi Stadi – SDL, VAT, Ushuru wa Stampu na huduma nyingine za kikodi. 

Akizungumza na walipakodi waliofika katika ofisi hiyo kupata huduma wakati wa uzinduzi, Bw. Kidata aliwashukuru kwa mwitikio wao katika zoezi la uhakiki wa taarifa za TIN ambao utaisaidia Mamlaka kupata idadi sahihi ya walipakodi ili kuondoa walipakodi hewa ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za ulipaji kodi.

“Zoezi hili litaongeza ufanisi katika suala zima la usimamizi na ukusanyaji kodi kwa kiwango cha juu” Alisema Bw. Kidata

Kamishna Mkuu wa TRA aliwataka walipakodi hao wanaoishi maeneo ya karibu na ofisi hiyo mpya ya TRA iliyopo Kimara Mwisho kuendelea kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma mbalimbali za kikodi ikiwemo uhakiki wa taarifa zao TIN kabla ya tarehe ya mwisho wa zoezi hilo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ni tarehe 30 Novemba 2016.

Aidha Kamishna wa Kodi za Ndani TRA Bw. Elijah Mwandumbya alisema TRA imejipanga kuhakikisha inaendelea kuboresha huduma zake na kuwafikia walipakodi kwa ukaribu zaidi ili kuondoa usumbufu na kuokoa muda wa upatikanaji wa huduma hizo.

“TRA kwa kuhakikisha walipakodi wanapata huduma iliyo bora imeanzisha vituo vingi vya kodi katika jiji la Dar es Salaam na nchi nzima ili walipakodi wapate huduma stahiki na ya haki na kuiwezesha Serikali kupata mapato yake kwa mendeleo ya Taifa letu” Alisema Bw. Mwandubya.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA) Bw. Alphayo Kidata – (Mwenye suti ya bluu katikati) pamoja na Kamishna wa Kodi za Ndani TRA Bw. Elijah Mwandumbya (Kushoto kwake) wakiwa katika picha ya pamoja na walipakodi waliofika katika Ofisi Mpya ya TRA Kimara ili kuhakiki Namba zao za Utambulisho wa Mlipakodi –TIN. Ofisi hiyo imezinduliwa leo tarehe 26 Oktoba 2016 na Kamishna Mkuu wa TRA ili kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi na kuboresha huduma mbalimbali za Kodi. 
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA) Bw. Alphayo Kidata akikata utepe kama ishara rasmi ya uzinduzi wa ofisi mpya ya TRA iliyoko Kimara Mwisho leo Tarehe 26 Oktoba 2016, Kushoto kwake ni Kamishna wa Kodi za Ndani TRA Bw. Elijah Mwandumbya pamoja na Wakurugenzi wengine wa TRA wakishuhudia tukio hilo 
Meneja wa TRA Kinondoni Bw. Wallace Mnkande (anayeongea kwa vitendo) akitoa maelezo ya kituo hicho kipya kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata (aliyeketi) wakati wa uzinduzi wa ofisi hiyo. Wengine kutoka kulia ni Kamishna wa Kodi za Ndani TRA Bw. Elijah Mwandumbya, Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani Bw. Abdul Zuberi, Meneja wa Majengo Gerald Mwikuka, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu Bw. Gerald Mwanilwa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo. 
Meneja wa TRA Kinondoni Bw. Wallace Mnkande akimwonesha jambo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata (kushoto kwake) alipotembelea ofisi ya TRA Kimara Mwisho wakati wa uzinduzi huo uliofanyika tarehe 26 Oktoba 2016 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...