Benki ya CRDB imesema
imeshangazwa na habari zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa iko mbioni
kufunga baadhi ya matawi yake kutokana na ukata.
Akizungumza na waandishi
habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Dkt. Charles Kimei alisema kuwa hakuna ukweli wowote kwenye taarifa hizo, kwani hivi
sasa Benki ya CRDB ipo kwenye hatua za mwisho za kufungua matawi mapya 11. Hii ikiwa ni muendelezo
wa sera yake ya kuhakikisha kuwa inafikisha huduma karibu zaidi na wateja.
“Nimeshangazwa sana habari hizi za upotoshaji, ukweli ni kuwa
mwaka jana (2015) tulifungua matawi 76 na kuajiri wafanyakazi 450. Mwaka huu (2016)
tumeshafungua matawi 51 na tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha matawi
mengine 11. Hii itafikisha jumla ya matawi
mapya 62 na jumla ya ajira mpya 600 kwa
mwaka huu tu. Takwimu hizi zinaonyosha kuwa Benki ya CRDB inaendelea kuimarika
na kuwa Benki kubwa zaidi nchini na katika ukanda huu wa Afrika Mashariki”.
Dkt. Kimei
aliyataja matawi hayo mapya kuwa ni Muheza na Handeni (Tanga), LAPF (Dodoma), Ruangwa
(Lindi), Soko la Mwanjelwa (Mbeya), Chato (Geita), Tarakea (Kilimanjaro), Mkwawa
(Iringa), Mikumi (Morogoro), Wete (Pemba) na Kigamboni-Dar es Salaam.
“Naomba kuwatoa hofu wateja wetu
juu ya taarifa zozote zenye lengo la kutuchafua kwani Benki ya CRDB iko vizuri na inategemea matokeo
makubwa ya kifedha ifikapo mwishoni mwa mwaka 2016” alisema Dokta Kimei.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...