KAMPUNI ya Isere Sports, inayojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya michezo, imejitokeza kulinogesha onyesho la 'Usiku wa Sikinde' kwa kutoa zawadi maalumu ya fulana.
Onyesho hilo, ambalo limelenga kuwakumbusha mashabiki nyimbo za zamani na mpya za bendi ya Mlimani Park Orchestra, linatarajiwa kufanyika Jumapili Novemba 27, mwaka huu, kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo,  Abbas Isere, alikabidhi fulana hizo jana, kwa Mratibu wa onyesho hilo, Rashid Zahor, katika hafla iliyofanyika ofisini kwake mjini Dar es Salaam.
Abbas alisema ameamua kutoa zawadi hiyo ya fulana ili kuiunga mkono bendi hiyo katika jitihada zake za kukuza na kuinua muziki wa dansi nchini.
"Mimi nimeishi sana mitaa ya Kariakoo na ni miongoni mwa mashabiki wakubwa wa Sikinde. Nilikuwa sikosekani kwenye kumbi ambazo bendi hii ilikuwa ikitumbuiza. Hivyo nimetoa fulana hizi kwa lengo la kuiunga mkono pamoja na nyinyi waratibu,"alisema. 
Mbali na kutoa zawadi hiyo ya fulana, Abbas alisema atakuwa miongoni mwa mashabiki watakaohudhuria onyesho hilo, ambalo amebashiri kuwa litakuwa la aina yake kwa sababu litakuwa kwa ajili ya watu maalumu.
Akipokea fulana hizo, Zahor alimshukuru Abbas kwa msaada huo, ambao alisema utalifanya onyesho hilo liwe na mvuto wa aina yake kwa sababu baadhi zitatolewa kwa mashabiki. Alisema wakati wa onyesho hilo, mashabiki watakaopendeza kwa mavazi, kucheza vizuri na kujibu vyema maswali yanayohusu Sikinde, watapatiwa zawadi hizo za fulana.
Baadhi ya nyimbo adimu zitakazopigwa kwenye onyesho hilo ni pamoja na Celina, Maudhi, Taraka rejea, Clara, Christina Bundala, Hiba, Barua kutoka kwa mama, Chenga ya mwili, Dua la kuku, Sitokubali kuwa mtumwa, Mtoto akililia wembe, Cenjesta na Epuka jambo lisilokuhusu. Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, aliwahakikishia mashabiki kwamba, watapata burudani murua na adimu, ambayo hawataisahau katika maisha yao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...