Na Ramadhani Ali, Maelezo           
Waandaaji wa michuano ya maadhimisho ya siku ya kisukari Duniani kwa Zanzibar Timu ya Wizara ya Afya imeyaaga mashindano hayo katika mchezo  wa ufunguzi baada ya kufungwa na timu ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na watoto kwa mikwajuni ya penelti katika kiwanja cha Amani nje.
Michezo hiyo inayoshirikisha Timu  nane za Wizara za Serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar  inachezwa kwa mtindo wa mtoano na fainali itachezwa tarehe 13 mwezi huu, siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho hayo yanayofanyika kili ifikapo 14 Novemba, ya kila mwaka.
Timu hizo zilimaliza dakika 90 zikiwa zimefungana bao 1-1 mabao yote yakipatikana kipindi cha kwanza . Wizara ya Kazi ilipata bao lake dakika ya 26 kupitia kwa mchezaji wao Ali Seif na  Wizara ya Afya ilisawazisha kwa njia ya penelti iliychongwa na Ahmed Rashid dakika ya 35.
Muda wa penelti tano-tano ulipowadia kila timu ilipoteza mbili na hatua ya kupigiana penelti moja moja ikaendelea na ndipo wenyeji wakajikuta wanapoteza penelti yao muhimu na kuipa michuano hiyo mkono wa kwaheri kwa masikitiko.
Akizindua michuano hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik Akili alisema lengo la maadhimisho ya siku ya kisukari duniani ni kuunga mkono jitihada za Kimataifa katika kupambana na maradhi hayo yanayoongezeka  kwa kasi duniani kote.
Alisema asilimia 3.7 ya Wazanzibari wanaugua maradhi ya kisukari na wengine wengi wako katika hatari ya kupata maradhi hayo iwapo hawatafanya juhudi za kujikinga.
Hata hivyo alisema tiba kubwa ya maradhi ya kisukari ni  watu kuweka utaratibu wa  kufanya mazoezi na kuweka utaratibu mzuri wa vyakula kwani ndiyo vinavyochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maradhi hayo.
Katibu Mkuu aliwashauri wafanyakazi wa Mawizara maidara taasisi za Serikali na binafsi na jamii kwa jumla kuhamasisha katika kufanya mzaoezi na kutenga wakati wa mapumziko ili kuweka mzunguruko mzuri wa damu na kupunguza uzito.
Timu zinazoshiriki michuano hiyo ni Wizara ya Afya, Wizara ya Kazi, Wizara ya Habari, Utalii Utamaduni na Michezo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko, Wizara ya Kilimo Maliasili Uvuvi na Mifugo na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. 
 Mratibu wa michuano ya maadhimisho ya siku ya Kisukari Duniani  Waziri Mohamed Ngwangwa akimuomba katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik  Akili kuzikagua timu ya Wizara ya Kazi na Wizara ya Afya katika ufunguzi wa michuano hiyo inayoendelea Kiwanja cha Amani nje Mjini Zanzibar.
 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik Akili akikagua timu ya Wizara ya Kazi na Wizara ya Afya kabla ya kuanza mechi ya ufunguzi wa mashindano ya maadhimisho ya siku ya kisukari Duniani katika  kiwanja cha Amani nje.
 Kikosi cha Timu ya Wizara ya Afya Zanziabar kabla ya pambano lao la ufunguzi.
 Kikosi cha Timu ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik Akili akitoa nasaha kwa wachaezaji wa timu ya Wizara ya Afya na Wizara ya Kazi  kabla ya kuanza mechi ya ufunguzi wa mashindano ya maadhimisho ya siku ya kisukari Duniani katika kiwanja cha Amani nje.
Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...