Mkurugenzi wa Mifumo Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Henry Katabwa ametaka Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) kuhusishwa kwenye michakato ya maendeleo ya serikali za mitaa, hasa kwenye programu zinazotekelezwa kwenye ngazi za chini kabisa ambapo ndiko wananchi wenye hali duni kimaendeleo wanapatikana. 
 
Kauli hiyo aliitoa wakati akifunga warsha ya malengo ya maendeleo endelevu kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Mipango kutoka mikoa saba ya kanda ya ziwa. Alisema malengo 17 ya maendeleo endelevu (SDGs) yamehusishwa kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano hivyo ni vyema kuhakikisha hata katika ngazi za chini utekelezaji wa program unazingatia malengo hayo.
 
 “Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, shabaha ya malengo haya inahusishwa kwenye michakato ya maendeleo ya serikali za mitaa na hasa kwenye miradi ya program zinazotekelezwa kwenye ngazi za chini kabisa, ambako ndiko wananchi wenye hali duni ya kimaendeleo wanapatikana” alisema .
Mwenyekiti wa warsha ya siku tatu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Mipango nchini ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi idara ya Mipango na Uratibu mkoa wa Mara, Eldom Anyosisye akitoa neno la ukaribisho wakati wa kufunga warsha ya siku tatu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Mipango nchini iliyomalizika mwishoni wa juma mjini Dodoma chini ya ufadhili wa Shirika UNDP.

Pia alisema serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na mradi wa uimarishaji wa wa sekta ya umma inaendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji takwimu ili uweze kukusanya takwimu katika ngazi zote za serikali za mitaa ili zitumike kuandaa mipango ya maendeleo. 
 
Akisoma maazimio kwa niaba ya washiriki wa warsha hiyo, Afisa Mipango wa wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Innocent Maduhu alisema sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 izingatiwe na kila mhusika atekeleze wajibu na majukumu yake. Pia yafanyike mapitio ya mgawanyo na matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwa lengo la kupata uhalisia sambamba na kuweka mkazo katika kutafuta rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.
Mkurugenzi wa Kupunguza Umaskini na Kuinua Uchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Anna Mwasha akizungumza jambo kabla ya mgeni rasmi kufunga warsha hiyo iliyomalizika mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.

Aidha wajumbe hao waliazimia kila sekta iwezeshwe vitendea kazi na rasilimali muhimu ili ziweze kutimiza majukumu yake pia mifumo ya upangaji mipango na utoaji taarifa ihuishwe ili iendane na Malengo ya Maendeleo Endelevu. Pia wametaka yafanyike mafunzo rejea ya mifumo kwa watumishi na kwa wakati na rasilimali katika sekta ya Kilimo ziongezwe kwa lengo la kuongeza na kuboresha uzalishaji na kupata malighafi kwa ajili ya viwanda. 
 
Sambamba na halmashauri zote kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya pamoja na kudhibiti mapato na matumizi, uwepo mpango au mkakati maalumu wa kuendeleza Mikoa na Halmashauri zilizopo nyuma kimaendeleo. “Mbinu za uibuaji na upangaji wa miradi ya maendeleo kutoka ngazi ya chini ufanyike upya katika halmashauri zote” alisema Maduhu.
Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Mifumo Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Henry Katabwa akitoa hotuba ya kufunga warsha ya siku tatu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Mipango nchini iliyomalizika mwishoni wa juma mjini Dodoma chini ya ufadhili wa Shirika UNDP.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...