Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 04 Novemba, 2016 kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani mwaka mmoja uliopita, amefanya mahojiano na Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mahojiano hayo yaliyorushwa moja kwa moja (Live) kupitia vyombo vya habari vya Redio, Televisheni na Mitandao yamechukua muda wa saa 2 na dakika 40 ambapo Rais Magufuli ametumia nafasi hiyo kujibu maswali yote yaliyoulizwa na wahariri na waandishi wa habari na ambayo yalilenga kujua utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha mwaka mmoja tangu iingie madarakani.

Katika majibu yake Rais Magufuli amesema katika kipindi cha mwaka mmoja Serikali yake imehakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, utulivu na umoja na pia imechukua hatua madhubuti za kuchochea kasi ya maendeleo zikiwemo kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Shilingi Bilioni 800 hadi kufikia wastani wa Shilingi Trilioni 1.2, Kununua ndege kwa ajili ya kurahisisha usafiri na kukuza sekta ya utalii, kuongeza bajeti ya maendeleo katika bajeti ya Serikali kutoka asilimia 26 hadi kufikia asilimia 40 na kujenga miundombinu ya barabara na madaraja.

Dkt. Magufuli amezielezea hatua nyingine kuwa ni kulipa madeni ya ndani na nje ya nchi, kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, kuongeza fedha za kununulia dawa na chanjo, kubana matumizi kwa kuelekeza fedha nyingi katika utatuzi wa kero za wananchi na kuimarisha uhusiano na ushirikiana na nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kuvutia uwekezaji katika viwanda, utalii, miundombinu na huduma za kijamii.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali imeweza kutoa fedha za ruzuku kwa shule za msingi na sekondari kiasi cha shilingi Bilioni 18.77 kila Mwezi kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa elimu bila malipo, imetoa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 148 kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi I na uanzishaji wa mradi wa umeme wa Kinyerezi II.

Kufuatia hatua hizo na nyingine nyingi, Rais Magufuli amesema katika mwaka mmoja wa uongozi wake nchi imeshuhudia ukuaji mzuri wa uchumi wa wastani wa asilimia 7.9 katika robo ya pili ikilinganishwa na asilimia 7 ya mwaka jana na kupunguza mfumuko wa bei kutoka zaidi ya asilimia 7 hadi kufikia asilimia 4.5 hivi sasa.

Dkt. Magufuli amesema amedhamiria kuhakikisha Serikali inarekebisha kasoro zilizokuwa zikisababisha upotevu wa mali ya umma, vitendo vya ulaji rushwa na uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka na kuijenga Tanzania mpya ambayo kila Mtanzania atanufaika na rasilimali za nchi yake.

Rais Magufuli ametoa wito kwa vyombo vya habari kufanya kazi zake kwa kutanguliza uzalendo, kuepuka kutumiwa na watu wenye nia ya kutetea maslai yao binafsi, kuepuka kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali kurekebisha kasoro zilizokuwa zikisababisha nchi kwenda vibaya.

Dkt. Magufuli amewapongeza Wahariri na Waandishi wa Habari kwa kazi kubwa wanayoifanya na amewaahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu utendaji kazi wa Serikali na maendeleo ya nchi yao.
  
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Novemba, 2016
 






Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akijibu maswali kutoka kwa wahariri wa vyombo mbalimbali aliokutana nao kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Dkt. Ayoub Rioba wakati wa kupokea  maswali kutoka kwa wahariri wa vyombo mbalimbali aliokutana nao kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsikiliza mwanahabari Sammy Awami wa BBC wakati akiuliza maswali kutoka kwa wahariri wa vyombo mbalimbali aliokutana nao kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi w3a mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsikiliza Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Serikali (TSN) Dkt. Jim Yonazi wakati akiuliza maswali kutoka kwa wahariri wa vyombo mbalimbali aliokutana nao kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi w3a mikutano wa Ikulu jijini Dar es  salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsikiliza Mtangazaji Tido Mhando wakati akiuliza maswali kutoka kwa wahariri wa vyombo mbalimbali aliokutana nao kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi w3a mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsikiliza Msanii Mrisho Mpoto akiimbwa wimbo wa "SIJONZE" wakati alipokutana na wahariri kwa mahojiano leo Ijumaa Oktoba 4, 2016 katika ukumbi w3a mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam.PICHA NA IKULU.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...