Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 03 Novemba,
2016 amekutana na Mwakilishi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania,
Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird na kuzungumzia utekelezaji wa miradi
ya maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani Bilioni
1.6 zikiwa ni mkopo kutoka benki hiyo.
Akizungumza baada
ya kumaliza mazungumzo yake na Rais Magufuli, Bi. Bella Bird amesema mikopo
hiyo inalenga kusaidia juhudi za maendeleo nchini Tanzania na itatolewa katika
sekta mbalimbali zikiwemo nishati, usafirishaji, elimu na maji.
"Miradi hii
yote imelenga zaidi kuharakisha maendeleo na kuleta matokeo katika maisha ya
Watanzania, ni miradi ambayo inahitaji uongozi na msukumo mzuri kutoka
Serikalini na tunafurahi kwamba Rais Magufuli ni kiongozi ambaye ana dhamira ya
dhati ya kusimamia maendeleo" amesema Bi. Bella
Bird.
Kwa upande wake
Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania
katika maendeleo na ametoa wito kwa Benki hiyo kuharakisha utoaji wa mikopo kwa
ajili ya kutekeleza miradi.
"Tunataka
kuona mambo yanatokea badala ya kutumia muda mwingi kuzungumza, miradi hii ina
manufaa makubwa kwa watanzania na tungependa utekelezaji wake ufanyike haraka,
na ili ufanyike haraka Benki ya Dunia inapaswa kutupatia mikopo kwa wakati
unaofaa" amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, Rais
Magufuli amemhakikishia Bi. Bella Bird kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano
imejipanga kusimamia utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa sasa na itakayoanza
kutekelezwa katika siku zijazo kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Kwa hivi sasa
miradi 26 yenye thamani ya Jumla ya Dola za Marekani Bilioni 4.5 inatekelezwa
hapa nchini kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
03 Novemba,
2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli akisalimiana na
Mwakilishi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia
Bi. Bella Bird Ikulu jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli akiagana na Mwakilishi
wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella
Bird mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...