Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 11 Novemba,
2016 amewaongoza viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuuaga mwili wa
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samuel John
Sitta aliyefariki dunia tarehe 07 Novemba, 2016 katika hospitali ya Technical
University of Munich nchini Ujerumani.
Mwili wa Marehemu
Samuel John Sitta umeagwa katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam ambapo
Viongozi wengine waliojumuika kuuaga mwili huo ni pamoja na Makamu wa Rais Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid, Rais Mstaafu wa Awamu
ya Tatu Mhe. Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Mawaziri wakuu
wastaafu Jaji Joseph Sinde Warioba na Frederick Tluway Sumaye, Katibu Mkuu
Kiongozi Balozi John Kijazi, Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Katipwa Wambali na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Baada ya kuagwa
katika viwanja vya Karimjee, mwili wa Marehemu Samuel John Sitta umesafirishwa
kwenda Dodoma ambako Wabunge, Viongozi wa Mkoa na wananchi watapata fursa ya
kuuaga katika Viwanja vya Bunge na baadaye jioni utasafirishwa kwenda Tabora
ambako maziko yatafanyika kesho Jumamosi huko Urambo.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo
cha Mbunge wa Jimbo la Dimani Zanzibar Mhe. Hafidh Ali Tahir kilichotokea
majira ya saa 9 usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.Mhe. Hafidh Ali
Tahir amefariki dunia muda mfupi alipofikishwa hospitali baada ya kuugua
ghafla.
"Nimeshtushwa
sana na kifo cha Mhe. Hafidh Ali Tahir na ninakuomba Mhe. Spika Job Ndugai
unifikishie salamu za pole kwa Familia ya Marehemu, Wabunge, Wananchi wa Jimbo
la Dimani, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote walioguswa na msiba huu.
"Tutamkumbuka
Mhe. Hafidh Ali Tahir kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika utumishi wa umma,
katika michezo na akiwa mwakilishi wa wananchi, kwa hakika tumepoteza mtu
muhimu sana" amesema Rais Magufuli na kumuombea
Marehemu apumzishwe mahali pema peponi. Amina.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
11 Novemba,
2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt . John Pombe Magufuli
akitoa heshima zake za mwisho kwa aliyekuwa Spika Mstaafu Marehemu
Samwel John Sitta alipoongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa
kiongozi huyo mkongwe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam
leo Novemba 11, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt . John Pombe Magufuli
akimfariji Mama Margareth Sitta, Mjane wa aliyekuwa Spika Mstaafu
Marehemu Samwel John Sitta alipoongoza mamia ya waombolezaji kuuaga
mwili wa kiongozi huyo mkongwe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es
salaam leo Novemba 11, 2016.
Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu Mhe Benjamin William Mkapa na mkewe Mama Anna Mkapa wakitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Spika Mstaafu Marehemu Samwel John Sitta alipoongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa kiongozi huyo mkongwe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Novemba 11, 2016
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Spika Mstaafu Marehemu Samwel John Sitta alipoongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa kiongozi huyo mkongwe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Novemba 11, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt . John Pombe Magufuli akimpa pole Mhe. John Sitta, mtoto wa aliyekuwa Spika Mstaafu Marehemu Samwel John Sitta alipoongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa kiongozi huyo mkongwe katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo Novemba 11, 2016.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...