Na Jacquiline Mrisho, Dodoma.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wamefanikiwa kuhamasisha baadhi ya wawekezaji kuwekeza katika sekta ya dawa za binadamu na vifaa tiba ili kupunguza uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi.

Hayo yamesemwa leo mjini Dodoma na Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Charles Mwijage alipokuwa akijibu swali la Mhe. Khadija Ali (Viti Maalum) aliyehitaji kufahamu mpango wa Serikali wa kutumia malighafi zilizopo kuzalisha baadhi ya dawa na vifaa tiba.

Waziri Mwijage amesema kuwa Serikali inaendelea na Mkakati Unganishi wa Maendeleo ya Viwanda (IIDS) pamoja na Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Miaka Mitano ambayo yote inalenga kuondoa changamoto ya kununua dawa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi.

“Serikali kupitia mashirika yake ya MSD, TIRDO, NHIF, TIB na TFDA wamepewa jukumu la kuandaa mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya dawa za binadamu pamoja na vifaa tiba kwa hiyo kupitia wizara yangu na TIC tayari tumefanikiwa kuwahamasisha wawekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani”, alisema Mwijage.

Baadhi ya wawekezaji hao ni JSN Solution ambao watajenga kiwanda cha kuzalisha IV Fluid, China Dalian International Economic Development Group Co. Ltd ambao watajenga kiwanda cha kutengeneza vifaa tiba, Zinga Pharmaceuticals Ltd pamoja na Hainan Hualon ambao watatengeneza madawa mbalimbali ya binadamu.

Waziri Mwijage amesema kuwa kupitia Ubalozi wa Korea nchini, Kampuni ya Boryung Pharmaceuticals Co. Ltd itatengeneza madawa ya Penicilin Orals Solids Antibiotics, wakati Agakhan Foundation Network watazalisha dawa mbalimbali.

Waziri Mwijage ameongeza kuwa kujengwa kwa viwanda vya dawa za binadamu na vifaa tiba kutakuwa na fursa pana ya kuwahakikishia Watanzania nafasi za ajira kwa vijana nchini kipindi kifupi kijacho.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage akijibu swali leo Bungeni mjini Dodoma 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...