Na Rhoda James.
Serikali
ya Tanzania na kampuni ya Ferrostaal Industrial GmbH kutoka Ujerumani
wamekutana kwa mara nyingine na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kutatua
changamoto zilizopo katika ujenzi wa Mradi wa kiwanda cha Mbolea wilayani Kilwa
Mkoa wa Lindi.
Katika
kikao hicho ambacho kimefanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, na ni
mwendelezo wa vikao vya aina hiyo vilivyotangulia, Naibu katibu Mkuu
anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo alizitaja changamoto
hizo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa ardhi na utambuzi wa bei ya kuuza gesi kwa kiwanda hicho.
Dkt.
Pallangyo alifafanua kuwa, utaratibu wa kupata ardhi kwa ajili ya Mradi huo
unaendelea vizuri kwani tayari Wananchi wamepata fidia ili kupisha Mradi huo na
kufikia Januari, 2017 Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) watakuwa
na hati mpya itakayoruhusu Kampuni ya Ferrostaal kuanza maandalizi ya ujenzi wa
kiwanda hicho.
Pamoja
na hilo pia Dkt. Pallangyo alisema kuwa bei ya gesi inajadiliwa na wadau
mbalimbali ikiwemo Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC), Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Shughuli za Mafuta (PURA), Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), wazalishaji wa gesi
(Upstreamer) na watumiaji wa gesi (Downstreamer) ili kujua bei halisi ya kuuza
gesi hiyo kwa kampuni ya Ferrostaal kwa kuwa inatarajia kutumia gesi katika
uzalishaji wa mbolea hiyo.
Kwa
upande wake Balozi wa Denmark Nchini , Einar H. Jensen alisema kuwa, ni vema
Bodi ya TPDC ikakamilisha utaratibu wa makubaliano ya ubia (Joint Venture
Agreement) kati yao na TPDC ili kuharakisha uanzishwaji wa utekelezaji wa mradi
huo.
Ujenzi
wa Mradi huo wa mbolea utashirikisha Kampuni tatu ambazo ni Ferrostaal
Industrial GmbH ya Ujerumani, Fauji Fertilizer ya Pakistani na Haldor Topsoe ya
Denmark pamoja na TPDC. Kikao
hicho kilishirikisha wawakilishi kutoka Kampuni ya Ferrostaal Industrial GmbH,
Viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na TPDC.
Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (mbele) akielezea jinsi Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ilivyojipanga kutekeleza ujenzi wa Mradi wa Kiwanda cha Mbolea wilayani kilwa. Balozi wa Denmark Nchini, Einar H. Jensen (kulia kwa Dkt. Pallangyo), Ujumbe kutoka Kampuni ya Ferrostaal Industrial GmbH Ujerumani, Viongozi Waandamizi kutoka Wizarani pamoja na Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wakimsikiliza Dkt. Pallangyo.
Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (mbele) akiwakilisha kabrasha ya kanuni za bei ya Gesi asilia kwa Balozi wa Denmark Nchini, Einar H. Jensen (mbele) wanaoshuhudia katika picha ni wajumbe kutoka Taasisi za Serikali pamoja na Ujumbe kutoka Kampuni ya Ferrostaal Industrial GmbH kutoka Ujerumani.
Balozi wa Denmark Nchini, Einar H. Jensen (aliyenyanyua mikono) akielezea mpango wao wa kujenga kiwanda cha mbolea wilayani Kilwa kwa washiriki kutoka upande wa Serikalini (hawapo pichani) wanaoonekana pichani ni Ujumbe kutoka kampuni ya Ferrostaal Industrial GmbH kutoka Ujerumani.
Viongozi Waandamizi kutoka Serikalini wakimsikiliza Meneja wa Biashara ya Gesi (Downstream) kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emmanuel Gilbert Simon wakati akielezea jambo katika kikao hicho
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...