KATIKA jitihada za kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwaandaa na kuwajengea uwezo wazalishaji wa viwanda wadogo na wakati, Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (SIDO),limepanga kuufanyia mabadiliko kimuundo shirika hilo ili kukidhi mahitaji wadau wake.

Mkurugenzi Mkuu, Profesa Sylvester Mpanduji amewaambia waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam kuwa mabadiliko hayo ya muundo yataweka mkazo zaidi juu ya kuimarisha viwanda na kuongeza uwekezaji.

“Mabadiliko haya ya kimuundo yatasaidia sana kutambua mahitaji ya wadau wetu,” alisema Prof.Mpanduji na kuongeza kuwa uhamasishaji wa viwanda na uwekezaji utasaidia mafanikio ya ajenda ya serikali ya awamu ya tano wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Prof. Mpanduji ambaye pia ni mhandisi, amesema watanzania na wajasiriamali wadogo na wakati wana mategemeo makubwa ya kuona SIDO imara yenye ufanisi na uwezo wa kuwahudumia wadau wake.

“Kutakuwa na mabadiliko makubwa ukilinganisha tulivyozoea utendaji wetu wa kufanya kazi. Tutatakiwa kwenda kuwafuata wazalishaji,kuwasikiliza na kuwasaidia huko,” alisema na kusisitiza kuwa ni lazima watu wabadilike kifikra pia. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Mkuu, mchango wa SIDO katika kufanya Tanzania nchi ya viwanda ni mkubwa na utaweza kupimwa kwa kuimarisha zaidi viwanda, kuongeza ajira zaidi pamoja na kuchangia mapato ya serikali.

“Nasikia fahari kusema kwamba shirika lina ofisi zake karibu kila mkoa Tanzania Bara isipokuwa katika mikoa ya Simiyu na Songwe,” alisema Prof. Mpanduji.

Alisema SIDO ina mchango mkubwa sana wa kufanya katika kuhakikisha azma ya serikali kuifanya nchi inakuwa ya viwanda inatimia.“Tunaunga mkono kwa vitendo dhamira ya serikali ya Awamu ya Tano yakuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na SIDO kwa kushirikiana na wadau wake tutafanya kila liwezekalo kufikia azma hiyo,” alisisitiza.

Lengo kubwa la SIDO ni kukuza viwanda vidogo vidogo nchini na kuchangia kupunguza umaskini,kukuza ajira, maendeleo ya biashara na kuchangia maendeleo ya uchumi kwa kuongeza kipato.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...