Na: Lilian Lundo – MAELEZO - SIMIYU

Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) katika shule za Msingi za Serikali Kata ya Migato, Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu umetatua kwa kiwango kikubwa tatizo la watoto wa kike kuacha shule na kwenda kuolewa.

Mratibu Elimu wa Kata hiyo Bw. Joshua Balomi, aliyasema hayo Mjini Bariadi alipokuwa akieleza mafanikio yaliyotokana na uanzishwaji wa UWW katika Shule za Msingi wakati wa semina ya mawasiliano na kushirikishana jitihada zenye mafanikio kwenye Elimu, inayoendelea Mjini Baridi.

“Mwaka jana, 2015 kata yangu ilikuwa na wanafunzi wa kike watatu ambao walikuwa na uwezo mkubwa darasani na walifanikiwa kufanya vizuri katika mitihani yao ya MOCK, cha kushangaza wanafunzi hao hao walifanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho ya kuhitimu Elimu ya Msingi.” alifafanua Balomi.

Uchunguzi ulifanyika na kubainika kwamba wanafunzi hao walirubuniwa na wazazi wao wafanye vibaya katika mitihani yao ya mwisho ili wasiendelee na masomo badala yake waende kuolewa.

Kamati za UWW zilishirikishwa juu ya tatizo hilo na kuchukua jukumu la kuongea na wanafunzi wa darasa la saba ambao wamehitimu masomo yao mwaka huu 2016 kwa kuwaambia umuhimu wa elimu na kuwatolea mifano ya wanawake waliofanikiwa kutokana na elimu waliyoipata.

Aidha kamati hizo ziliwahusia wanafunzi hao kutokubali kujifelisha ili waende kuolewa badala yake wazazi wanapowashauri kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho kutofuata ushauri huo kwani elimu wanayoipata ni kwa ajili ya maisha yao wenyewe na sio kwa ajili ya wazazi wao.

Juhudi hizo za UWW zilizaa matunda ambapo katika matokeo ya darasa la Saba ya mwaka huu 2016 wanafunzi wote wa kike waliotegemewa kufanya vizuri katika kata hiyo walifanya vizuri kama ilivyotarajiwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...