Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imetangaza dhamira yake ya kuuza hisa kwa umma itakayofuatiwa na kujiunga kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya Elektroniki na Mawasiliano ya Posta (EPOCA) na sheria ya Fedha ya mwaka 2016 ambayo inaelekeza makampuni ya simu kumilikisha asilimia 25 ya hisa zake kwa wananchi kwa kujiunga na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Akizungumzia hatua hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Bwana Ian Ferrao (pichani) alisema “Tunayo furaha kutangaza kuwa tumeanza rasmi mchakato wa kuuza hisa kwa umma kwa mujibu wa matakwa ya sheria na tumewasilisha maombi na utaratibu mzima utakaotumika kuuza hisa zetu na ratiba yetu nzima kuhusiana mchakato huu kwenye Mamlaka ya Usimamiaji wa Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa (DSE). Hatua hii ni kubwa na inadhihirisha kuwa Vodacom ipo mstari wa mbele katika kutekeleza agizo la kuuza hisa zake kwa umma na inadhihirisha jinsi ilivyojipanga kuendelea kuboresha na kukuza sekta ya mawasiliano nchini Tanzania katika siku za usoni”.
Uuzaji wa hisa kwa umma na kujiunga na Soko la Hisa kunapitia hatua mbalimbali za kupata vibali kutoka taasisi za serikali zenye mamlaka ya kupitia maombi na kutoa vibali vya utekelezaji wake.Ferrao aliendelea kueleza “Tunaamini uuzaji wa hisa zetu kwa umma utazidi kukuza shughuli za Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE),kunufaisha watanzania kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.Kampuni yetu haitajulikana kwa jina la mwanzo la Vodacom Tanzania Limited bali imekuwa na jina la
Vodacom Tanzania Public Limited Company (Plc) ikiwa ni hatua ya awali ya kujiandaa kuingia sokoni. Tunawahakikishia kuwa mchakato wa kuingia kwenye hatua hii umeanza vizuri kwa mafanikio na tunaendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali kutoka serikalini kuhakikisha tunatimiza dhamira ya kuanza kuuza hisa kwa wananchi yenye dira ya kuleta manufaa kwa wote.”
Ferrao alitoa msisitizo kuwa Vodacom inalo jukumu kubwa kuhakikisha hatua hii inaleta manufaa kwa pande zote zinatazohusika kuanzia wanunuaji wa hisa, kuendelea kuwekeza , kuendelea kuleta mapinduzi ya ubunifu wa kiteknolojia na kuimarisha ubora wa huduma za kampuni kwa wateja wake “Tutaendelea kutoa mchango mkubwa wa ufanikishaji wa sera ya nchi ya miaka 5 ya kukuza sekta ya mawasiliano.Tutaendelea pia kuwaletea taarifa mbalimbali kuhusiana na mchakato wa kuuza hisa kwa umma unavyoendelea”Alisema Ferrao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...