Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana amemtumia salamu za rambi rambi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es salaam Ndg. Ramadhan Madabida kufuatia kifo cha Muasisi wa TANU Bibi Hadija Bint Kamba, kilichotokea jana tarehe 30 Novemba, 2016 jijini Dar es salaam.

Bibi Hadija Bint Kamba ni miongoni mwa wanaharakati waliopigania uhuru na ukombozi wa Taifa letu. Ameshiriki kuanzisha Baraza la Wanawake Tanganyika mwaka 1955 na baadae Umoja wa Wanawake wa Tanganyika (UWT) tarehe 02 Novemba 1962 akishirikiana na Bibi Titi Mohamed.

Bibi Hadija hakuwahi kushika nafasi za uongozi ndani ya Chama na Serikali baada ya uhuru mpaka mwaka 1985 ambapo Mwalimu Nyerere alimtangaza mbele ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Baraza la Wazee wa Dar es salaam Diamond Jubilee, kuwa ni mtu aliyetoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Chama na Nchi, tangu wakati huo Bibi Hadija Bint Kamba alihudhuria Mikutano mikuu ya Chama kama mjumbe mwalikwa mpaka umri ulipomzuia kuweza kushiriki.

Bibi Hadija Binti Kamba, atakumbukwa na wanachama wa CCM kwa uadilifu, uvumilivu, ujasiri na mchango wake mkubwa katika ujenzi na uimarishaji wa Chama chetu, na kwamba mchango wake katika kupigania uhuru na kuleta ukombozi na maendeleo kwa Wanawake wa taifa hili utaendelea kuenziwa na kuthaminiwa na Watanzania.

Hakika sisi ni wa MwenyeziMungu na kwake yeye ndio marejeo yetu. 

Imetolewa na:- 


Christopher Ole Sendeka (MNEC)
MSEMAJI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
01.12.2016

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...