WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuacha tabia ya kuhifadhi fedha nyingi
majumbani na badala yake wajenge utamaduni wa kuzipeleka benki kuepusha
kuhatarisha usalama wao.
Ametoa
ushauri huo jana (Jumatatu, Desemba 5, 2016) wakati akifungua tawi la benki ya
Biashara ya Uchumi lililopo wilayani Karatu mkoani Arusha akiwa katika ziara
yake ya kikazi mkoani hapa.
Alisema
tabia ya baadhi ya wananchi kuhifadhi kiasi kikubwa cha fedha majumbani si
nzuri kwa sababu wanahatarisha usalama wao, hivyo ni vyema wakatumia benki
mbalimbali zilizoko kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutunza fedha zao.Akizungumzia
kuhusu kufunguliwa kwa tawi la benki ya Uchumi wilayani Karatu, Waziri Mkuu
alisema unaashiria ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo kwa kuwa benki ni kichocheo
cha maendeleo.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliushauri uongozi wa benki
ya Uchumi kuangalia uwezekano wa kupunguza kiasi cha riba wanachokitoza katika
mikopo wanayoitoa ili kuwawezesha wananchi kukopa na kupata tija.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Bw. Wilson Ndesanjo
alisema benki hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mtaji mdogo
jambo linalowasababisha washindwe kufungua matawi katika mikoa mingine.
“Changamoto
nyingine ni baadhi ya wateja kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati, ambapo
hatua za kisheria zikichukuliwa wanakimbilia mahakamani. Matukio haya
yanadhoofisha kasi ya utoaji wa huduma kwani kesi zinachukua muda mrefu,”
alisema.
Bw.
Ndesanjo alisema kuna baadhi ya kesi zimechukua miaka sita bila ya kumalizika
hivyo kuzuia fedha ambazo kama zingerejeshwa kwa wakati zingezungushwa kwa
wananchi wengine.
Benki
ya Uchumi ilianzishwa Septemba 22, 2005 ikiwa na mtaji wa sh. milioni 372. Hadi
kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2016 mtaji huo umefikia sh. bilioni 5.4
hivyo umeongezeka mara 14.5 zaidi ya ule wa awali uliokuwepo wakati wa
uanzishwaji wake.
IMETOLEWA NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU
JUMANNE,
DESEMBA 6, 2016.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...