Na Is-haka Omar, Zanzibar.

KATIBU wa Idara ya Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar,  Waride Bakari Jabu amesema chama hicho kitaendelea kuishauri serikali na kutumia rasilimali zake katika kusimamia sera na mikakati yake katika  kuimarisha huduma na fursa za kimaendeleo kwa wananchi.

Alisema malengo hayo yatafikiwa endapo wafuasi wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla watawaunga mkono, kuwaamini na kuwachagua  wagombea wanaopeperusha bendera ya CCM kwa kila uchaguzi wa kisiasa ili waweze kuwaletea wananchi maendeleo kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho.

Hayo aliyasema wakati akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari juu ya maandalizi ya ufungaji wa Kampeni za Chama hicho katika Uchaguzi mdogo wa jimbo la Dimani Unguja, alisema maandalizi ya kufungwa kwa kampeni hizo yamekamilika kwa kufuata miongozo, ratiba na masharti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo alisema  Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dr. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa kampeni hizo zitakazofanyika  Januari 21 mwaka huu kuanzia majira ya saa 8:00 mchana  katika Kiwanja Cha Shule (Skuli) ya Fuoni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

Alisema Dr. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar atawahutubia wananchi kwa kueleza sera, mikakati na muelekeo wa utekeleza wa shughuli za kimaendeleo zilizotekelezwa na Chama hicho na zinazotarajiwa kutekelezwa katika maeneo mbali mbali nchini hasa katika jimbo la Dimani.

Katibu huyo alisema viongozi wengine watakaohudhuria Kampeni hizo na kupewa fursa ya kuzungumza na wafuasi wa Chama hicho ni Katibu Mkuu wa CCM  Taifa, Abdulrahman Omar Kinana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai pamoja na viongozi na watendaji ngazi mbali mbali za taasisi hiyo.

Aidha alisema matarajio ya CCM katika Uchaguzi wa Jimbo hilo ni kuendeleza ushindi wa kihistoria kutokana na wananchi wa rika mbali mbali kumkubali mgombea wa Chama hicho, Juma Ali Juma na kuahidi siku ya uchaguzi watamchagua rasmi bila pingamizi awe Mbunge wa jimbo hilo.

“ Tunawaomba wafuasi wetu na wananchi kwa ujumla mjitokeze kwa wingi katika Mkutano wa Ufungaji wa kampeni za CCM kesho (leo) ili muweze kusikiliza sera na mipango endelevu inayotekelezeka kwa vitendo itakayoelezwa kuwa ufasaha na Dr. Shein pamoja na viongozi wengine.

Pia wale ambao ni wakaazi na wapiga kura halali wa Jimbo la Dimani  tuendelee kuhamasishana nyumba kwa nyumba ili siku ya uchaguzi Januari 22 mwaka huu, tujitokeze kwa wingi katika vituo vya kupigia kura kwa lengo la kumpa ridhaa Juma Ali Juma aweze kuwatumikieni kupitia vipaumbele vyake.”, alieleza Waride na kuongeza kuwa CCM ndio Chama pekee kinachotambua thamani na utu wa makundi yote ya kijamii yaliyopo nchini.

Hata hivyo aliwasihi wafuasi wa CCM kufuata utaratibu na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoashiria vurugu na uvunjaji wa kanuni za wapiga kura siku ya uchaguzi badala yake wale waliotimiza umri wa kupiga kura na wamekamilisha taratibu zote kisheria wafike mapema katika vituo kwa kupiga kura na kurudi nyumba kusubiri matokeo.

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani Unguja, Hafidh Ali Twahir kufariki Dunia ghafla mwaka uliopita  akiwa katika utekelezaji wa Majukumu yake huko bungeni Mjini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...