WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi Wazara wa Elimu Sayansi na Telnolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda mkoani Mtwara kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha shule tisa za mwisho katika matokeo ya kidato cha pili kutoka mkoani humo.
Pia ameziagiza halmashauri nchini kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili kuhakikisha wanawasimamia vizuri walimu jambo litakalowezesha kuboresha ufundishaji na hatimaye kupata matokeo mazuri.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Januari 17, 2017) wakati akizungumza na watumishi na wananchi wa mkoa wa Katavi alipowasili Ikulu ndogo ya Mpanda kwa ajili ya kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Kwa mujibu wa matokeo hayo kati ya shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo, tisa zinatoka katika Mkoa wa Mtwara na moja Tanga. Shule za Mtwara zilizofanya vibaya ni Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na Lukodoka  huku ya Tanga ikiwa ni Nywelo.
“Viongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waende Mtwara wakafuatilie kwa kina wajue kuna nini hadi shule tisa kati ya 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili mwaka jana zitoke huko,” amesisitiza.
Mbali na kuuagiza huongozi wa wizara hizo kwenda mkoani Mtwara pia Waziri Mkuu amewataka wasimamie vizuri mikoa ambayo awali ilikuwa na matokeo mabaya na sasa inafanya vizuri na wahakikishe shule za mikoa hiyo hazishuki na badala yake ziendelee kupata matokeo mazuri zaidi.
Awali, akisoma taarifa ya mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga alisema katika matokeo ya mtihani kidato cha pili ya mwaka jana mkoa wake ulishika nafasi ya pili kitaifa ukiongozwa na mkoa wa Geita.
Alisema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha katika mitihani ya mwaka huu wanashika nafasi ya kwanza kitaifa, hivyo alitoa wito kwa watendaji wa Idara ya Elimu, wakuu wa shule, wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JANUARI 17, 2017.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...