Imeelezwa kuwa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) utaanza rasmi kutekelezwa mwezi Februari mwaka huu. Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo mjini Dodoma wakati akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Ameongeza kuwa, katika utekelezaji wa Mradi huo, Serikali imepanga kuwakabidhi Wakandarasi watakaotekeleza mradi huo kwa Wabunge ili kuhakikisha kwamba mradi husika unatekelezwa kikamilifu.

Wakati huo huo, Kamati hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake Dotto Biteko imeipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa ukusanyaji wa Maduhuli kwa kipindi cha nusu mwaka na kueleza kuwa, mwelekeo wa ukusanyaji huo unakwenda vizuri.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akijibu hoja za Wabunge wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa wizara hiyo Dkt. Medard Kalemani na Kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Justin Ntalikwa wakifuatiwa na viongozi wengine wa Wizara na Taasisi zake.

Awali, akiwasilisha Taarifa ya Wizara ya Nishati na Madini kuhusu upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha nusu mwaka kwa Kamati, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Profesa Justin Ntalikwa, ameeleza kuwa, hadi kufikia Disemba 31, 2016 Wizara ilikuwa imekusanya jumla ya shilingi bilioni 201.86 sawa na asilimia 54.46 ya lengo lililokusudiwa.

“ Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato hayo yanatokana na vyanzo mbalimbali vikiwemo ada za kijiolojia, mrahaba, ada za mwaka za leseni, mauzo ya nyaraka za zabuni, mauzo ya gesi asilia, tozo ya mauzo ya umeme na shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia,”amesema Prof. Ntalikwa.
Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zilizo chini ya Wizara wakiwa katika kikao cha maandalizi na kwa ajili ya vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini siku moja kabla ya kuanza kwa vikao hivyo.

Aidha, akieleza utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa kipindi cha Julai hadi Disemba, 2016 Prof. Ntalikwa amesema kuwa, Wizara imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati kulingana na mpango wake na kuitaja miradi kadhaa ikiwemo mradi wa Kusafirisha Umeme Msongo wa kilovoti 400 kutoka iringa hadi Shinyanga na kueleza kuwa, ulikamilika tarehe 28 Disemba,2016.

“ Mradi wa Kinyerezi II wenye Megawati 240 utekelezaji wake umefikia asilimia 29 na Serikali imekwishatoa mchango wake wote wa asilimia 15 sawa na shilingi bilioni 110 na mradi huu unategemewa kukamilika mwaka 2018,” amesisitiza Prof. Ntalikwa.

Akizungumzia Mradi wa Kinyerezi I, Extension ya Megawati 185 ambao ni mwendelezo wa upanuzi wa Mradi wa Kinyerezi 1, ameeleza kuwa, mradi huo unaendelea kutekelezwa na unatarajiwa kukamilika mwaka 2018.

Akizungumzia uendelezaji wa Uchimbaji Mdogo, Prof. Ntalikwa amesema kuwa, ili kukuza utendaji wao, Wizara inaendelea na hatua za uanzishwaji wa vituo vya mfano vitano katika Wilaya za Kilwa, Mpanda, Chunya na Bukoba kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Ameongeza kuwa, vituo hivyo vitatumiwa na wachimbaji hao kuchenjua madini yao na kujifunza namna bora ya kuendesha migodi yao kitaalam na kwa tija zaidi.
Kaimu Kamishna wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati ya Nishati na Madini, Mhandisi Innocent Luoga, wa kwanza kulia akifuatiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Felix Ngamlagosi, na Mtaalamu kutoka Ewura wakibadilishana jambo kabla ya kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Watendaji Wakuu wa wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini wakifuatilia jambo wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMIZO), Mhandisi Hamisi Komba akijibu hoja ya Wajumbe wa kamati wakati wa kikao kati ya Wizara na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini mjini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...