Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa juhudi kubwa walizofanya kunusuru maisha ya Bi. Neema Mwita Wambura ambaye alijeruhiwa kwa kuunguzwa na maji ya moto kifuani, shingoni na mkononi.
Pongezi hizo za Mhe. Dkt. Magufuli zimetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bw. Gerson Msigwa muda mfupi baada ya kumfikisha Neema Mwita Waitara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako Rais Magufuli ameagiza apelekwe kwa mara nyingine kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa maendeleo ya afya yake.
Katika Pongezi hizo Mhe. Dkt. Magufuli amesema Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefanya kazi kubwa na ya kizalendo kuhakikisha Neema anapona licha ya majeraha makubwa aliyoyapata miaka miwili iliyopita na ambayo yalitishia uhai wake.
Pia Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mama Mariam Amir (Bibi Mwanja) kwa upendo wake wa kumchukua Neema na kisha kumpa hifadhi nyumbani kwake huko Tandika Devis Kona Jijini Dar es Salaam.
“Nakushukuru sana Mama na ninakupongeza, umeonesha mfano mzuri wa kujali umoja na upendo kwa Watanzania wenzako bila kujali dini, kabila wale kanda unayotoka na hivi ndivyo Watanzania wote tunapaswa kufanya” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Dada Neema Mwita Wambura (32) akizungunza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kupitia njia ya Simu akimshukuru kwa msaada aliompatia wa kufanyiwa tena uchunguzi wa afya yake katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Pia Rais Dkt. Magufuli ameahidi kumpatia hifadhi mama huyo pamoja na watoto wake watatu ambao kwa sasa wapo Bunda mkoani Mara. Pia Rais Dkt. Magufuli alimpatia msaada Dada huyo kiasi cha Shilingi laki tano. Dada Neema Mwita Wambura aliungua vibaya mara baada ya kumwagiwa uji wa moto uliokuwa unachemka jikoni na mume wake katika kijiji cha Kyagata, Tarime mkoani Mara.
Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakimpokea Dada Neema Mwita Wambura (32) na kuanza mara moja kumfanyia tena uchunguzi wa afya yake katika majeraha aliyoyapata mara baada ya kumwagiwa uji wa moto uliokuwa ukichemka jikoni kitendo kilichofanywa na mume wake.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Profesa Lawrence Museru akimjulia hali Dada Neema Mwita Wambura (32) mara baada ya kufikishwa tena hospitalini hapo. Dada Neema Mwita alifanyiwa upasuaji mara nne katika siku za nyuma hospitalini hapo Muhimbili ili kutibu majeraha yake hayo ya moto.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya dharura na Ajali katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Juma Mfinanga akizungumza kuhusu hali ya mgonjwa Dada Neema Mwita Wambura (32) aliyefikishwa tena katika Hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi wa Afya yake.
Daktari Bingwa wa upasuaji wa ngozi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Ibrahim Mkoma akizungumzia historia ya mgonjwa huyo ambaye yeye pamoja na jopo la madaktari bingwa walimfanyia upasuaji ili kutibu majeraha yake ya ngozi katika kipindi cha nyuma. PICHA NA IKULU.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...