Na Mbaraka Kambona, 
Ujumbe wa Tume inayohamasisha umoja na mshikamano  na kupambana na aina zote za utengano wa Makabila kwa jamii ya watu wa Kenya ( National Cohesion and Integration Commission) umesema kuwa wanatamani kuiona Kenya inakuwa kama Tanzania ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliijenga katika misingi ya umoja na mshikamano.
Wakiongea katika kikao kifupi baada ya ujumbe huo kufanya ziara katika ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora jijini Dar es Salaam,ujumbe huo haukusita kueleza hisia zao juu ya Tanzania na kueleza  kuwa  suala la Ukabila nchini Kenya bado lipo na ndio moja ya mambo ambayo wanashughulika nayo.
“Tungetamani sana Kenya ingekuwa kama Tanzania, kwani Mwalimu aliijenga Tanzania kuwa taifa moja” alisema  Kamishna Dzoro, na kuongeza: “Tunasikia wivu kwenu...Tanzania imejengwa kama Taifa sisi Kenya bado ni nchi”, aliongeza Profesa Gitile
Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Bahame  Nyanduga wakati akiwaeleza kuhusu majukumu ya tume,  pia aliwaomba kwamba, kwa kuwa wanaelekea katika uchaguzi mkuu wahakikishe vyama vya nchini kwao vinajihepusha na kuunda vikundi vya vijana wa chama “youth league” ambavyo kwa uzoefu uliopatikana katika uchaguzi  uliopita nchini Tanzania  vikundi hivyo vilianza kujiingiza katika majukumu ambayo sio yao ya kutaka kulinda maeneo ya kupigia kura na kulinda kura jambo ambalo ni hatari kwa  amani na usalama wa nchi.
Ujumbe huo wa watu wanne ulioongozwa na Kamishna, Mhe. Morris Dzoro ulikuwa na lengo la kujifunza namna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wanavyofanya kazi zake.
Wajumbe wengine waliokuwa katika ziara hiyo ni  Kamishna, Profesa Gitile Naituli,  Mkurugenzi wa Programu, Bi. Millicent Apondi Okatch na Afisa wa elimu ya uraia na uhamasishaji, Ndugu Richard Nderitu.
NCIC ilianzishwa kwa lengo la kuhamasisha umoja na mshikamano katika jamii ya watu wa Kenya  kwa kuandaa michakato na sera mbalimbali zinazowezesha kuondoa aina zote za ubaguzi wa kikabila nchini humo.
 Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Bahame Tom Mukirya Nyanduga (kulia) akiongea katika kikao kifupi na ujumbe wa Kamisheni  inayohamasisha umoja kwa jamii ya watu wa Kenya na kuondosha aina zote za utengano wa makabila (National Cohesion and Integration Commission - NCIC) ya nchini Kenya uliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam  kwa lengo la kujifunza namna tume inavyofanya kazi zake. Ujumbe huo uliongozwa na Kamishna, Mhe. Morris Dzoro (kushoto), wa pili kushoto ni Kamishna, Profesa Gitile Naituli, wa tatu kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Programu, Bi. Millicent Apondi Okatch. 
 Mkurugenzi wa Programu, Bi. Millicent Apondi Okatch akiongea katika kikao kifupi baina ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na National Cohesion and Integration Commission (NCIC), kulia anayeandika ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Bahame Tom Mukirya Nyanduga.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Bahame Tom  Nyanduga (kulia) akiongea na Makamishna wa NCIC mara baada ya kumaliza kikao. Kushoto ni Kamishna, Mhe. Morris Dzoro na katikati ni Kamishna, Profesa Gitile Naituli.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...