Na Mary Gwera, Mahakama
KAIMU Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof.  Ibrahim Juma ameutaka Uongozi mpya wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuusoma na kuuelewa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ili umoja huo uweze kuchangia katika utekelezaji wake.
Prof. Juma aliyasema hayo mapema leo, Ofisini kwake, Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam alipotembelewa na Uongozi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) ukiongozwa na Rais wa Chama hicho, Mhe. Tundu Lissu.
Alisema kuwa ni vyema kuusoma Mpango Mkakati huo ili kufahamu ni wapi Mahakama inatoka na wapi inapotaka kuelekea hususani katika suala zima la maboresho ya huduma ya utoaji haki nchini.
Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2015/2016-2019/2010) umegawanyika katika nguzo kuu tatu ambazo ni Utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali,  Upatikanaji na utoaji haki kwa wakati na Kurejesha imani ya jamii na ushirikishwaji wa wadau,  umejikitika katika kuboresha huduma za utoaji haki kwa ujumla.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), amemueleza Mhe. Kaimu Jaji Mkuu kuwa lengo la ujio wao ni kujitambulisha kwake na pia kumpa pongezi Mhe. Kaimu Jaji Mkuu kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Mbali na utambulisho, Mhe. Tundu Lissu alipata wasaa wa kueleza baadhi ya changamoto zinazowakabili Mawakili nchini ikiwa ni pamoja na baadhi ya Mahakama kutokuwa na Ofisi kwa ajili ya Mawakili, taratibu za usajili wa Mawakili n.k
Akijibu kuhusu hoja ya Rais wa TLS; Msajili; Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ilvin Mugeta alisema kuwa Mahakama Kuu inaendelea kufanyia kazi changamoto zote zinazowakabili Mawakili na vilevile kuona uwezekano wa taratibu za malipo kufanyika kielektroniki.
 Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma (aliyeketi mbele) akiwa pamoja na baadhi ya Viongozi wapya wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) waliomtembelea kwa lengo la kujitambulisha kwake kama Uongozi mpya na pia kumpongeza Mhe. Kaimu Jaji Mkuu kwa uteuzi wake, aliyeketi kushoto kwa Mhe. Kaimu Jaji Mkuu ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali na aliyeketi kushoto kwa Kaimu Jaji Mkuu ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Mhe. Tundu Lissu.
 Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akiongea jambo na Uongozi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) walipomtembelea Ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha.
 Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Mhe. Tundu Lissu akiongea jambo, Ofisini kwa Mhe. Kaimu Jaji Mkuu walipofika kwa ajili ya utambulisho wa Uongozi  mpya wa Chama hicho.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania (wa sita kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) walipomtembelea Ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha, wa tano kushoto ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, wa kwanza kushoto ni Msajili, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ilvin Mugeta na wa tano kulia ni Rais wa Chama hicho, Mhe. Tundu Lissu.(Picha na Mary Gwera)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...