Na Husna Saidi-MAELEZO

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Kimataifa la Jinsia na Usawa Katika Jamii lililoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) Aprili 27 mpaka 28 mwaka huu chuoni hapo.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Chuo hicho Lila Mandu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu lengo la kongamano hilo.

Mandu alisema lengo kuu la kongamano hilo ni kuchunguza kwa kina masuala mbalimbali ya kijinsia pamoja na kubaini mbinu bora za kuondoa ukosefu wa usawa wa jinsia katika muktadha wa Taasisi za Elimu ya Juu.

“Tutatathmini sababu na changamoto zinazosababisha ukosefu wa usawa wa kijinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu kwa kutumia mifano mizuri kutoka Taasisi zingine ambazo zinajitahidi kuhamasisha usawa na haki za wanawake na wanaume pia,” alisema Mandu.

Aliendelea kwa kusema kuwa kongamano hilo litabainisha fursa za kimkakati katika kuwahusisha wadau wa masuala ya jinsia katika kuhamasisha usawa na haki za watu wote ambapo litakuwa na washiriki 140.

Aliwataja washiriki hao kuwa ni wasomi kutoka DUCE, Taasisi na vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi, wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu katika masuala ya jinsia, wawakilishi wa mashirika ya haki za binadamu, watunga sera pamoja na wasomi wanaotambulika Kimataifa katika masuala ya jinsia.

Kwa upande wake, Mratibu Kitengo cha Jinsia DUCE Fatma Hamad alisema licha ya maovu wanayotendewa wanawake kuendelea kujitokeza hapa nchini, kongamano hilo litasaidia kutoa elimu ya jinsia na usawa ili kusaidia Serikali na wananchi kwa ujumla kuondokana na hadha hiyo.

Chuo cha DUCE pamoja na waandaaji wa kongamano hilo wamealika wadau mbalimbali wa masuala ya jinsia, wasomi, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kushiriki katika kongamano hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...