Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii.

Kesi dhidi ya mfanyabiashara, Ndama Shabani Hussein maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto ya Ng'ombe imeamliwa kuendelea kusikilizwa baada ya mshtakiwa huyo kukana baadhi ya maelezo ya awali (PH), licha ya mwanzoni mwa wiki hii kukubali shtaka la utakatishaji wa fedha kiasi cha USD 540,000.

Mapema wiki hii, Ndama alikiri kutenda kosa hilo ambalo ni kosa la sita kati ya anayoshtakiwa nayo, na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikapanga leo iwe siku ya kusomewa maelezo ya awali (PH), kabla ya kumsomea hukumu yake.

Hata hivyo, wakati akisomwa Maelezo hayo na wakili wa serikali Christopher Msigwa Ndama alikana baadhi ya tuhuma na kukiri chache kitendo kilichofanya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Victoria Nongwa kuamuru kesi hiyo iendelee kama kawaida kwani tuhuma alizokataa mshtakiwa ndizo zinajenga msingi wa kesi.

Ndama anayetetewa na Wakili Jeremiah Mtobesya alikiri baadhi ya maelezo ya awali aliyosomewa na wakili wa Serikali Msigwa ikiwamo nyaraka zilizotumika kufungua akaunti iliyotumika kuingizwa hizo fedha, hundi zilizotumika kutolea hizo fedha, maelezo ya benki ‘bank statement’ na Swift massage.

Hata hivyo alikana baadhi ya maelezo ambayo ni sehemu ya kuunda shtaka hilo, na kusema kuwa hawajui wakurugenzi wa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited wanaotambulika Brela, Bushoboka Mutamura na Mujibu Hamis Taratibu.

Aidha alikanusha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited haikuwahi kuingia mkataba na Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited  na kwamba hakuwahi kuwagaia wabia wenzake fedha hizo taslimu kwa lengo la kuficha chanzo chake.

Baada ya mshtakiwa kukana baadhi ya PH Msigwa alidai mahakamani hapo kuwa kwa kuwa mshtakiwa alikuwa amekiri kosa ni rahisi kuthibitisha yaliyofanyika na kwamba kwa kadiri maelezo ya awali yalivyosomwa na majibu ya mshtakiwa basi ni jukumu la mahakama kuangalia kama maelezo aliyokubali yanakidhi kumtia hatiani ama kesi ianze kusikilizwa.

“Ili haki ionekane imetendeka na kwa vile mshtakiwa anakubali baadhi ya maelezo na mengine ameyakataa mahakama inaona ni vema kesi ianze kusikilizwa ili kila upande upate haki yake kwani mshtakiwa alitakiwa akubali shtaka hili bila ya kupinga lakini kwa kuwa amekana baadhi ya tuhuma ni wazi kuwa amekana shtaka”, amesema Hakimu Nongwa.

Baada ya kutolewa kwa amri hiyo, Msigwa ameiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Kesi itatajwa tena Juni 6, mwaka huu.

Mei 16, 2017, Ndama alikubali shtaka la sita la kutakatisha fedha ambapo anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014, Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye  benki ya Stanbic alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa dola za Marekani 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la kujiapatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mashtaka mengine anayokabiliwa nayo ni kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...