Na Ramadhan K. Dau
Siku ya Jumatano tarehe 24 Mei 2017 ni siku ambayo itakumbukwa na Watanzania wengi na haswa Waislamu kwa kuondokewa na mzee wetu Alhaj Kitwana Selemani Kondo maarufu “KK” au mzee wa mjini. 

Siku 4 kabla ya kifo chake, mwanawe wa kiume Bwana Adnan Kitwana Kondo maarufu “Saku” alinitumia ujumbe kwenye WhatsApp akiniarifu kuwa mzee KK amelazwa Hindu Mandal na hali ya afya yake inazidi kuzorota. Siku ya pili yake nilimtumia ujumbe “Saku” kutaka kujua hali ya mzee inaendeleaje. Majibu ya “Saku” yaliniashiria kuwa mzee wetu amekaribia kufika mwisho wa safari yake. Aliniambia kuwa kwa sababu ya ukaribu wangu na mzee KK hana budi aniarifu ukweli ulivyo. Aliniarifu kuwa hali ya mzee ni mbaya sana na kwamba kinachosubiriwa ni Rehma Zake Mwenyezi Mungu. Kwa kweli ujumbe ule ulihuzunisha sana na sikuweza kuhimili uchungu ule peke yangu. Nikamwarifu Profesa Hamza Mustafa Njozi, Makamu Mkuu wa Chuo cha Waislamu Morogoro na Bwana Faraji Abdallah Tamim, mwalimu wa chuoni hapo.

Ilipofika siku ya Jumatano tarehe 24 Mei nikapata taarifa kupitia moja ya kundi sogozi (chat group) kuwa mzee KK amefariki dunia. Pamoja ya kuwa hali hiyo ilikuwa tayari inatawala fikra zangu lakini kifo hakizoeleki.  
Moja kati ya sifa zake nyingi ni ujasiri. Mzee KK hakuwa mwoga na alikuwa na ujasiri wa kusimamia jambo ambalo anaamini ni sahihi na lina manufaa kwa nchi yetu. Mifano iko mingi. Kwa leo itoshe tu kuwa alisimamia suala la upatikanaji wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro kwa kujenga hoja kwa Rais wa wakati huo Mhe Benjamin William Mkapa mpaka Mhe Rais akashawishika kuwa ni jambo jema kuanzishwa kwa chuo hicho kwenye majengo ya kilichokuwa Chuo cha Mafunzo cha TANESCO.
(Pichani ni Mhe Mkapa akiwa na KK kushoto kwake na viongozi wengine waliohudhuria sherehe ya kuzindua uanzishwaji wa Chuo cha Kiislamu Morogoro).  

Kama kuna mtu mmoja ambaye ametoa mchango wa kipekee uliopelekea upatikanaji wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) mtu huyo ni mzee Kitwana Kondo. 


Kwa kuenzi jitihada zake hizo, na kwa kuzingatia mzee Kondo ni Mwenyekiti mwanzilishi wa Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF), taasisi ambayo ndiyo Mmiliki wa MUM, nashauri uongozi wa Chuo utafute jengo lenye hadhi pale Chuoni lipewe jina lake. Kwa siku za usoni, Chuo kitakapoanza kutoa shahada za Uzamivu (PhD), nashauri mzee Kitwana Kondo atunukiwe PhD (Honoris Causa) posthumously.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...