Na Nteghenjwa Hosseah – Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Daqaro amesema wanawake na vijana wanaokidhi vigezo wapewe Zabuni za Halmashauri ya Jiji ili kuweza kuwainua kiuchumi na kuboresha maisha yao kwa kazi mbalimbali zinazotolewa kila mwaka.
Daqaro ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wanawake na vijana ambao ni wajasiriamali wanaonufaika na mikopo yenye riba nafuu kutoka Jiji ambayo hutolewa kwa mujibu wa sheria.
 “Ni wakati wa wanawake na vijana kuchangamkia fursa mbalimbali katika Jiji la Arusha ikiwa ni pamoja na zabuni ambazo zitasaidia kuinua mitaji na kuongeza pato la familia zenu, hizi kazi ni zenu hakikisheni mnafuata taratibu zote ili mzichukue wasije watu toka mbali wakapewa wakati ninyi ambao ni wakazi wa Mji huu mkakosa kwa kukosa vigezo vidogo watumieni wataalamu wa Jiji wawaelimishe”amesema Daqaro.
Wakati akisema hayo Mkuu wa Wilaya Mhe. Daqaro amekabidhi hundi za mfano ya Tsh Mil 390 kwa vikundi vya wanawake 78 huku vikundi vya vijana 67 vimekabidhiwa hundi ya Tsh Mil 336.
Mhe. Daqaro amesema kuwa kutokana na changamoto iliyoko katika taasisi za fedha ambazo hutoa mikopo kwa riba kubwa na kuhitaji dhamana ya nyumba na ardhi jambo ambalo linawakwamisha wakopaji hivyo Serikali imeamua kutoa mikopo ya masharti nafuu ambayo ni asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Pia amewasihi wanufaika wa mikopo hii kuwa mikopo itumike katika malengo maalumu na katika miradi inatakayoleta tija kama vile uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo ambavyo vitasaidia kutengeneza ajira na kukuza uchumi.
Kwa upande wao kinamama na vijana waliopokea mikopo hiyo wamesema kuwa mikopo hiyo itawainua kiuchumi na kuwawezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali na kuachana na kuwa tegemezi pamoja na matumizi ya dawa za kulevya  na wizi.
Mpaka kufikia robo ya tatu Machi 2017 Halmashauri ya jiji la Arusha imetoa mikopo ya Tsh Bil 1.3 kwa ajili ya wanawake  na vijana kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
  Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Fabian Daqarro (katikati) akifungua mafunzo ya wajasiriamali yanayoenda sambamba na utoaji wa mikopo ya wanawake na vijana kwa robo ya tatu.
Mkurugezi wa Jiji la Arusha Ndg. Athumani Kihamia (tatu kulia) akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa wajasiriamali ambao ni wanufaika wa mikopo ya Halmashauri ya Jiji kwa robo ya tatu.
  Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Fabian Daqarro (katikati) akiwakabidhi hundi ya mfano ya Tsh Mil 390 kwa vikundi vya wanawake Jiji la Arusha.
 Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Fabian Daqarro (katikati) akikabidhi hundi ya mfano ya Tsh Mil 336 kwa vikundi vya vijana, Jiji la Arusha.
 Washiriki wakifuatilia mafunzo ya ujasiriamali kabla ya kukabidhiwa mikopo ya riba nafuu toka Jiji la Arusha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...