Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh bilioni 32.5 ya kodi ya majengo, kwa mwaka wa fedha 2016/17 kutoka katika Majiji, Miji na Manispaa 30 nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) amewaambia waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kwamba makusanyo hayo ni sawa na asilimia 56 ya lengo lililowekwa Mwaka wa Fedha uliopita la kukusanya shilingi bilioni 58.
Alisema kuwa hatua niyo ni mafanikio makubwa tangu TRA ipewe jukumu la kukusanya kodi hiyo ambapo mwaka wa fedha 2015/2016 katika maeneo hayo, Halmashauri zilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.3 wakati TRA imekusanya kiasi hicho cha shilingi bilioni 32.5 tangu ianze kukusanya kodi hiyo mwezi Oktoba mwaka wa fedha 2016/2017.
“Mpaka kufikia tarehe 15 Julai mwaka huu TRA imekusanya sh. bil 32.5 kipindi ambacho ni kifupi, na kwamba mapato hayo yanatarajiwa kuongezeka kutokana na mwitio mkubwa wa wananchi kulipa kodi ya majengo”Alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango aliwapongeza wananchi kwa mwitio wao mkubwa wa kulipa kodi ya majengo na kwamba wameonesha uzalendo wa kweli na ndio maana Serikali imeamua kuongeza muda wa kulipa kodi hiyo bila adhabu hadi Julai 30 mwaka huu, hali anayoamini itapandisha zaidi mapato hayo.
Katika hatua nyingine Dkt, Philip Mpango aliwapongeza wamiliki wa vituo vya mafuta waliotii maagizo ya Serikali, kwa kufunga mashine stahiki za EFDs, akitolea mfano vituo vya PUMA na TOTAL ambavyo vimefunga mashine hizo kwenye pampu zao zote.
Aliwaonya wamiliki wote wa vituo vya mafuta ambao hawatafunga mashine hizo za EFDs ndani ya siku 14 kama agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli linavyoelekeza na kwamba yeye kama Waziri mwenye dhamana atahakikisha analisimamia kikamilifu na kwamba baada ya muda huo mtu asijekuilaumu Serikali baada ya kuanza kuchukua hatua kali za kisheria.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akivipongeza Vituo vya Mafuta vya Puma na Total kwa kuonesha mfano wa kufunga mashine za EFDs katika Pampu zote za mafuta kwenye vituo vyao, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.(Picha: Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akiwaomba wananchi kulipa kodi ya Majengo mapema kwa mwaka wa Fedha 2017/18 ili kuepuka usumbufu wa msongamano, alipofanya Mkutano na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akitoa agizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha kuwa mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFDs) zinatumika ipasavyo na kutengenezwa mara moja zinapoharibika na kwamba zisipotengenezwa ndani ya saa 48 zifungwe na wamiliki wake watozwe faini, alipozungumza na wanahabari, Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...