Mkurugenzi wa shule St Anne Marie iliyoko Mbezi kwa Msuguri jijini Dar es Salaam, Jasson Rweikiza akimpa zawadi mwanafunzi bora wa darasa la saba, Katherine Mujungi, kwenye mahafali ya darasa la saba ya shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki maeneo ya Mbezi kwa Msuguri jijiini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
 IMEELEZWA kuwa uwekezaji bora kwenye sekta ya elimu, ikiwamo miundombinu, maktaba na walimu walio na sifa za kufundisha, itaongeza ufaulu na uelewa kwa wanafunzi.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa shule ya St. Anne Marie, Jasson Rweikiza kwenye mahafali ya 18 ya wanafunzi wa darasa la saba, yaliyofanyika shuleni hapo Mbezi kwa Msuguri.

Alisema ili kuinua kiwango cha ubora wa elimu nchini, ipo haja ya kuzingatia uwekezaji huo pamoja na kuboresha maslahi ya walimu kwa kuwa watapata ari ya kufundisha.

"Shule ikiwa na mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia kama vile vifaa vya kutosha, madawati, maji, maktaba, walimu wenye ari matokeo ni elimu bora, wadau tuwekeze zaidi," alisema Rweikiza ambaye ni Mbunge wa Bukoba Vijijini na Mwenyekiti wa wabunge wa CCM.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Gradius Ndyetabula alisema shule binafsi ni muhimu kwa kuwa zinatoa mchango wa elimu na kuongeza fursa kwa Watanzania.

 Alisema iwapo shule za serikali pekee zingeachiwa mzigo wa elimu vijana wengi wangekosa fursa ya kujiunga na kuendelea na masomo, kutokana na uchache wa shule za serikali.

 Alieleza shule hiyo imeshika nafasi ya 32 kitaifa matokeo ya darasa la saba yaliyopita kati ya shule za msingi 16,350 na kwamba wanatarajia wahitimu 43 wa darasa la saba mwaka huu watafanya maajabu kwasababu maandalizi waliyofanya ni mazuri.

Alisema kwenye matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karibuni, St Anne Marie ilifanikiwa kuwa ya tano  kwenye Mkoa wa Dar es Salaam kwenye matokeo hayo lakini siri kubwa ni mfumo mzuri wa ufuatiliaji wa matokeo ya wanafunzi kitaaluma kuanzia ngazi za chini.

Alisema pia shule hiyo ilifanikiwa kuwa ya kwanza kwa Wilaya ya Ubungo jijini hapa na hivyo kuziacha kwa mbali shule zaidi ya 11 zenye kidato cha tano na sita wilayani humo.

Aidha, alisema mbali na kushika nafasi ya tano kwa Mkoa wa Dar es Salaam, shule hiyo ilifanikiwa kufaulisha wanafunzi 15 kwa daraja la kwanza, wanafunzi 48 daraja la pili, wanafunzi 23 daraja la tatu na mwanafunzi mmoja tu ndiye aliyepata daraja la nne.

“Dar es Salaam kuna shule 56 zenye kidato cha tano na sita na nyingi zinavifaa na zana za kufundishia hivyo sisi kupenya hadi kuwa namba tano si jambo rahisi, sisi tumejipanga kwa walimu wazuri na mazingira bora ya kusomea kama maktaba ya kisasa na tunaahidi kufanya maajabu kwenye mitihani ijayo,” alisema Ndyetabula.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...