Mwanza, Agosti 20, 2017: Shirika la Taifa la hifadhi ya Jamii (NSSF) limetoa mkopo wa Tshs bilioni 8.99 kwenda kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ya Tanzania kwa ajili ya ufufuaji wa kiwanda cha usindikaji wa nafaka katika jiji la Mwanza ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za mfuko huo kutekeleza kwa vitendo sera ya uchumi wa viwanda hapa nchini.

Mkopo huo unalenga kuiwezesha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kuweza kuvifufua vinu vyake viwili vya usindikaji wa mazao ya mpunga na mahindi vilivyopo mkoani humo kwa  kununua vifaa na mitambo mipya na hatimaye kuanza uzalishaji baada ya kusimamisha uzalishaji huo mapema miaka ya 1990.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya hundi ya mkopo huo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Mwanza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Jenista Mhagama alitoa wito kwa Wizara yenye dhamana ya kulimo hapa nchini kuisimamia vyema bodi hiyo kiutendaji ili iweze kuijendesha kwa ufanisi utakaoiwezesha kurejesha mkopo huo unaotarajiwa kulipwa ndani ya kipindi cha miaka sita (6) ikijumlisha kipindi cha mpito yaani (grace period) ya mwaka mmoja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Jenista Mhagama (wa pili kushoto) Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Taifa la hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara (kulia) ikiwa ni mkopo kutoka Shirika hilo kwenda bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko kwa ajili ya ufufuaji wa kiwanda cha usindikaji wa nafaka kilichopo jijini Mwanza. 

"Mbali na Wizara yenye dhamana ya kilimo, pia niwaombe sana uongozi wa mkoa wa Mwanza chini ya Mkuu wa mkoa kutambua kuwa ufanisi wa kiwanda hiki unategemea sana uwepo wa malighafi ya kutosha hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha uwiano kati ya uzalishaji wa malighafi na uzalishaji wa kiwanda vinakwenda sambamba,'' alisisitiza. 

Alilipongeza Shirika la NSSF  kwa uwekezaji wa viwanda vyenye tija kiuchumi ndani ya muda mfupi ambapo kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja uliopita hadi sasa shirika hilo limewekeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kiwanda cha kutengeneza viuadudu vya kuua vimelea vya mbu kiitwacho Tanzania Biolarvicide Limited kilichopo Kibaha, mkoani Pwani.

"Uwekezaji wa NSSF pia unaonekana kwenye bodi ya nafaka na Mazao mchanganyiko ya Tanzania, Mkoani Dodoma, viwanda vipya vya kuzalisha sukari Mkulazi, mkoani Morogoro, kiwanda cha chaki Maswa (Maswa Chalk & General Enterprises) ambacho kipo Simiyu...hongereni sana!'' alipongeza.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Jenista Mhagama akikabidhi mfano wa hundi hiyo kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba (kushoto) huku wadau wengine wakishuhudia.

Waziri Mhagama alitumia wasaa huo pia kuwataka  waajiri wasiolipa michango ya wanachama kuwasilisha michango hiyo kwa wakati na kwa usahihi kwani  kutofanya hivyo ni kosa kisheria na  kuanwanyima haki wanachama hao huku akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wale wasiotekeleza sharia hiyo.


Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alimuhakikishia Waziri Mhagama kuwa mbali na kuisimamia kwa ukaribu bodi hiyo ili iweze kurejesha mkopo huo, wizara yake imejipanga kuhakikisha kwamba miradi yote ya kilimo inayohusisha uwekezaji kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii hapa nchini inasimamiwa kwa umakini, ufanisi na weledi mkubwa ili kulinda pesa ya wanachama wa mifuko hiyo.

"Kwa kutambua kwamba ufanisi wa viwanda hivi unategemea zaidi kilimo kuna mipango na mikakati mizuri kuhakikisha mnyororo wa thamani unaohusika kuzalisha malighafi za viwanda hivi haukatiki,'' alisema Waziri Tizeba.
Kabla ya makabidhiano hayo Waziri Mhagama alipata wasaa kukugua mitambo ya kinu cha kukoboa mchele kinachotarajiwa kufufuliwa kupitia mkopo huo ambapo Mtendaji mkuu wa bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko Bw. John Maige (mbele) alimuhakikishia Waziri Mhagama na wadau wengine kuwa kufufuliwa kwa kiwanda hicho kutawezesha jumla ya tani 96 za mchele kukobolewa kwa siku kupitia kinu hicho.

Alitaja baadhi ya mipango na mikakati hiyo kuwa ni pamoja na ujio wa Mpango maalumu wa kuandaa mbegu bora unaotekelezwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Bill Gates. Alikili kuwa kwasasa taifa linakabiliwa na uhaba wa mbegu bora unaotakona na utegemezi wa mbegu hizo kutoka nje ya nchi huku taifa likizalisha asilimia 35 tu ya mbegu hizo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...