Na Mbeya Yetu
Vigogo 6 kati ya 12 wanaotuhumiwa kuhusika kwenye kashifa ya ufisadi wa soko la Kimataifa la Mwanjelwa jijini Mbeya wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mbeya na kusomewa mashtaka matatu ya uhujumu uchumi.
Waliopandishwa kizimbani Mahakamani hapo ni aliyekuwa Meya wa jiji hilo, Athanas Kapunga (70)  aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji hilo, Elizabeth Munuo (65) na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji hilo Dk. Samwel Lazaro ambaye kwa sasa ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe. 
Wengine ni aliyekuwa Mtunza Hazina wa Jiji hilo, James Jorojik (62), aliyekuwa Mwasibu wa jiji hilo, Tumaini Msigwa (47) na Mhandisi wa jiji hilo, Emily Maganga (42). 
Mwendesha mashtaka wa serikali, Shadrack Martin, akisaidiwa na Hebel Kihaka pamoja na Baraka Mgaya wakati akiwasomea mashtaka yanayowakabili vigogo hao alisema wote kwa pamoja walitenda makosa ya uhujumi uchumi kati ya mwaka 2008 na 2013 hivyo kuisababishia serikali hasara kubwa.
Katika Shtaka la kwanza mwendesha mashtaka huyo alisema linawahusu watuhumiwa waili ambao ni Athanas Kapunga ambaye alikuwa Meya wa Jiji la Mbeya na Elizabeth Munuo ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji ambao wanadaiwa kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya Shilingi Bilioni 3.3, ambapo wanadaiwa kusaini mkopo wa kiasi hicho cha fedha kutoka katika Benki ya CRDB ambao ulianza kulipiwa riba kabla ya kuanza kujengwa kwa Soko hilo la Mwanjelwa kinyume cha vifungu vya sheria namba 57 (1) na 60 (1)  na (2)  vya Sheria za uhujumu uchumi Sura ya 200 ya mwaka 2002.

Martini alisema shtaka la pili linawahusu Dk.Samwel Lazaro, James Jorojik, tumain Msigwa na Emily Maganga ambao kwa pamoja wanadaiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuidhinisha malipo ya shilingi milioni 304,470,500 kwa Mkandarasi aliyekuwa anajenga soko hilo, Nandhra Engineering and Constaction ltd wakati kazi hiyo ilikuwa tayari imefanywa na Kampuni ya Tanzania Building Works ltd.

Aidha  Washtakiwa wa Shataka namba mbili pia wanashtakiwa kwa kosa la tatu la kuisababishia Halmashauri ya Jiji hasara ya shilingi 1,140,228,750 kwa kuidhinisha malipo ya fedha hizo kwa wakandarasi Tanzania Building Works na Nadhra Engineering kwa ajili ya ujenzi wa Soko hilo wakati kazi iliyotajwa haikuwemo kwenye Mkataba.

Washtakiwa hao kwa pamoja walikuwa wakitetewa na Mawakili watatu wakiongozwa na James Kyando, Baraka Mbwilo na Secilia Luhanga ambao waliiomba Mahakama hiyo kutoa maelezo kuhusu uwezekano wa wateja wao kupata dhamana. Hata hivyo Mwendesha Mashtaka wa serikali alisema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo akaiomba mahakama kupanga siku nyingine kwa ajili ya kutajwa tena.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mbeya, Michael Mteite alisema Mahakama haina uwezo wa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi hivyo washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu hadi Agosti 29, Mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Kufikishwa Mahakamani kwa vigogo hao kunatokana na agizo la Waziri mkuu alilotoa Julai 31 mwaka huu wakati wa ziara ya kikazi jijini hapa alipozungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na Jiji na kuwataja wahusika 13 waliotajwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  (CAG) na kupendekeza wachukuliwe hatua.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...