WAZIRI wa Maliasili na Utalii Prof Jumanne Maghembe mwishoni mwa wiki hii alizindua rasmi usajili wa msimu wa nane wa mbio za Rock City Marathon huku akiahidi kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo katika kuhakikisha kuwa zinatumika vema kuutangaza utalii wa ndani.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya uzinduzi huo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa mchezo huo wakiwemo viongozi wa serikali pamoja na wadhamini mbalimbali wa mbio hizo, Waziri Maghembe alisema azma yake hiyo inasukumwa na malengo ya mbio hizo ambayo ni kutumia mchezo wa riadha katika kutangaza utalii hususani katika Ukanda wa Ziwa.

"Kwa kuzingatia uzito wa malengo ya mbio hizo nitamke bayana kuwa nipo tayari kushirikiana na waandaaji wa mbio hizi kuhakikisha kwamba kuanzia mwaka huu mbio hizi zinafana na zinavutia washiriki wengi zaidi hususani wa kimataifa,'' alisema Waziri Maghembe ambae pia alithibitisha ushiriki wake kwenye mbio hizo zinazoratarajiwa kufanyika Octoba 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na kupita katika barabara mbalimbali za jiji hilo kabla hazijamalizikia katika uwanja huo.

Mbali na ushiriki wake,Waziri Maghembe alitoa wito kwa mashirika mbalimbali yaliyo chini ya wizara yake ikiwemo la Hifadhi za Taifa(Tanapa), Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Makumbusho ya Taifa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kufanikisha mbio hizo.

"Ukanda wa Ziwa una vivutio vingi ambavyo pia kama Wizara yenye dhamana ya utalii lazima tuvigeukie na kuvitangaza kwa nguvu na kwa njia tofauti ikiwemo michezo,'' alisema Waziri Maghembe huku akivitaja baadhi ya vivutio hivyo kuwa ni pamoja na Kisiwa cha Saanane, Makumbusho ya kabila la Wasukuma pamoja na tamaduni za makabila ya wakazi wa Kanda ya Ziwa.

Mbio za Rock City Marathon zilizoanzishwa miaka minane iliyopita zinazozidi kujiongezea umaarufu kila mwaka na tayari zimefanikiwa kuwavutia baadhi ya wadhamini ikiwa ni pamoja na kampuni za TIPER, PUMA, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),Mwanza Hotel , Real PR Solutions Limited, Afrimax Strategic Partnerships Limited, EF Outdoor, CF Hospital na ATCL. 
 WAZIRI wa Maliasili na Utalii Prof Jumanne Maghembe akizungumza na wadau mbalimbali wa mchezo wa riadha hapa nchini pamoja na waandaaji wa mbio za Rock City Marathon kwenye hafla maalumu ya uzinduzi  rasmi usajili wa msimu msimu wa nane wa mbio hizo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam. 
 Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo, Bw Zenno Ngowi akizungumza kwenye hafla hiyo. Alitoa wito kwa washiriki wa ndani hususani wa mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na wadhamini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo ambazo kwa mwaka jana zilifanikiwa kuhusisha washiriki zaidi ya 2000 na watazamaji zaidi ya 30,000. 
 Mratibu wa mbio hizo zinazoandaliwa na kampuni ya Capital Plus International, Bi Adeline Ndesanjo akitoa maelezo kuhusu maandalizi ya mbio hizo kwenye hafla hiyo. Alisema mbio za mwaka huu zinatarajiwa kuhusisha washiriki wengi zaidi kutoka kila kona ya dunia ikiwemo Afrika, Ulaya,China,Mashariki ya Kati hususani Israel na Marekani . 
 Wadhamini nao hawakuwa nyuma!Meneja Masoko wa Kampuni ya mafuta ya Puma Energy, Bw Machumani Shebe alisema ushiriki wao kwenye mbio hizo umechagizwa zaidi na azma ya kampuni yake hiyo kuisaidia serikali katika kuutangaza utalii wa ndani. 
 Baadhi ya wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Prof Jumanne Maghembe akiwa kwenye picha ya pamoja na waandaaji wa mbio hizo pamoja na wadau mbalimbali wa mchezo huo wakiwemo  viongozi wa serikali pamoja na wadhamini wa mbio hizo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...