NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo amefanya ziara ya kukagua miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na kuahidi kuwa serikali itafanya ukarabati wa baadhi ya majengo haraka iwezekanavyo.

Akizungumza mara baada ya kukagua miundombinu ya hospitali leo mjini Dodoma, Jafo amesema hospitali hiyo ndio kimbilio la watu wengi na kwamba baadhi ya majengo yake yanahitaji kufanyiwa maboresho ili yaendane na hadhi ya Makao makuu ya Nchi.

Amesema majengo hayo yamejengwa tangu enzi za Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ni ya zamani hivyo yanatakiwa kufanyiwa maboresho ili yawe ya kisasa na kwamba serikali inajipanga kufanya maboresho hayo na kwa kuanzia itapeleka Sh.milioni 500 kuanza ukarabati katika jengo la upasuaji.

Ameeleza jengo la upasuaji ni la muda mrefu na miundombinu yake kwa ndani haiendani na hali ya sasa na kwamba inatakiwa kukarabatiwa ili iwe ya kisasa.“Serikali tutaleta fedha ili tukarabati jengo hili liendane na hali halisi ya mahitaji hasa ikizingatiwa Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi hivyo ni kimbilio la watu wengi,”amesema Jafo

Aidha amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa Dk.Charles Kiologwe na uongozi wa hospitali hiyo kuanza mchakato wa kuwasilisha maombi serikalini kwa ajili ya kuboresha majengo ya hospitali hiyo ambayo asilimia kubwa yalijengwa wakati Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Kadhalika, amepongeza ujenzi wa jengo jipya la kisasa la akina mama na watoto na kuagiza ujenzi wake ukamilishwe kabla ya mwisho wa mwezi wa oktoba mwaka huu kwa kuwa serikali imeshapeleka fedha za ukamilishaji.

Aidha amepongeza ujenzi wa jengo la wagonjwa wa Bima ya Afya na kwamba linapokea wagonjwa wengi kwa siku kutokana na ubora wa miundombinu yake.Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Caroline Damian amesema jengo hilo limekuwa likitumika kufanya upasuaji kwa wastani wa watu 500 kwa wiki.

Naye, Mganga Mkuu Dk. Kiologwe amesema miundombinu ya hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1929 na kwamba licha ya changamoto ya miundombinu lakini huduma za afya zimekuwa zikitolewa kwa ufanisi.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa na viongozi mbalimbali wa serikali katika ukaguzi wa jengo la Akinamama na watoto katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua miundombinu ndani ya jengo la upasuaji katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk.Charles Kiologwe akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo alipokuwa akikagua chumba cha kufulia nguo za Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akitoa maelekezo kwa wakandarasi wa ujenzi wa jengo la Akinamama na watoto alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...