RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza haja kwa Ofisi ya Mufti pamoja na viongozi wa misikiti ya kisasa inayojengwa hapa nchini kuwa na mikakati mizuri ya uendeshaji na uangalizi kwani baadhi ya misikiti hiyo iliyojengwa kwa gharama kubwa imekuwa ikipoteza haiba yake kutokana na uchakavu.

Alhaj Dk. Shein alisema kuwa misikiti hiyo ya kisasa iliyojegwa kwa gharama kubwa imekuwa ikipoteza haiba na kukumbwa na chamgamoto ya uchakavu wa miundombinu muhimu baada ya kipindi kifupi tangu inapokabidhiwa kwa Kamati za Misikiti au wananchi wa maeneo yanayohusika.

Hayo ameyasema leo katika  ufunguzi wa msikiti wa Jaamiu Zinjibar  ambapo katika  hotuba yake ya ufunguzi wa msikiti huo , Alhaj Dk. Shein alisisitiza kuwa kila inapowezekana ni vyema Ofisi ya Mufti ikawa na ufuatiliaji wa misikiti hiyo inayojengwa kwa gharama kubwa ili kuangalia utunzaji na maendeleo yake.

Aliongeza kuwa miradi ya ujenzi wa misikiti inayojengwa na ikatunzwa vizuri na kwa uadilifu, huwa wanatiwa moyo wale wenye nia na ari ya kusaidia na kuzidi kufungua milango ya kheri, neema na riziki kwa Waislamu wa maeneo mengine ambao bado hawajafaidika na neema kama hiyo.

Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani za dhati kwa Serikali ya Oman kwa kukubali kujenga msikiti huo mkubwa, mzuri na wa kisasa hapa Zanzibar na kutoa shukurani kwa wananchi wa Oman chini ya uongozi imara wa Sultan Qaboos Bin Said Bin Al Said.

Pia, Dk. Shein alimpongeza Balozi Mdogo wa Oman aliyopo Zanzibar Dk. Ahmed Hamoud Al Habsi na wasaidizi wake kwa juhudi walizochukua hadi mradi huo ukakamilika kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Aidha, Alhaj Dk. Shein alisisitiza haja ya kuitumia misikiti ipasavyo na kujiepusha kufanya mambo yanayoweza yakawa shirki sambamba na kujiepusha na mizozo pamoja na mifarakano ambayo haina tija kwa Waislamu.

Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa kwa bahati mbaya katika miaka ya hivi karibuni, kuna baadhi ya Waislamu katika baadhi ya misikiti walianza kugombania uongozi wa misikiti, walikuwepo waliotishia kuiteka misikiti kwa kuwa katika himaya yao na baadhi yao walifanya uharibifu wa vifaa na nyenzo.

Aliongeza kuwa wapo waliodiriki kuwafukuza waumini wenzao na kugawana makundi ya waliokuwa na haki na wasiokuwa na haki ya kuongoza na wengine walipoanzisha mizozo yao walidiriki hadi kupigana na kuumizana kwani walighafilika juu ya umuhimu wa msikiti na mwenye msikiti.

Alieleza imani yake ni kwamba msikiti huo wa Jaamiu Zinjibar utakuwa ni miongoni mwa kiungo muhimu cha kuwaunganisha Waislamu wa Zanzibar kutokana na jina uliopewa na kuwa kitovu muhimu katika kutekeleza ibada ya funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kukumbushana umuhimu wakutekeleza Hijja.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwahimiza wananchi na waumini wanapopata bahati ya kuwaleta wadhamini na wafadhili wa ujenzi wa misikiti na madrasa na uchimbaji wa visima, wawafikishe wafadhili hao katika sehemu za vijijini, Unguja na Pemba ili nao wazidi kupata neema hiyo kwani misikiti na madrasa nyingi za kisasa bado zinajengwa katika maeneo ya mjini ikilinganishwa na vijijini.

Pia, Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa Waislamu wote washirikiane katika kujenga madrasa wao wenyewe badala ya kukaa na kusubiri wafadhili katika kutekeleza ibada hiyo muhimu huku akiwataka wazazi kuwa na moyo wa kushirikiana na walimu wa madrasa katika kusomesha na kuwalea watoto.

Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mmanga Mjengo Mjawiri alitoa pongezi kwa Serikali ya Falme ya Oman na hasa Sultan Qaboos  kwa msaada wa TZS Bilioni 17.9 ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechangia eneo la ujenzi, msamaha wa kodi wa vifaa vyote vya ujenzi vilivyotoka nje ya nchi na msamaha wa malipo ya mkandarasi sawa na TZS Bilioni 3.1.

Mkataba wa ujenzi wa Msikiti huo ulitiwa saini tarehe 6 Januari mwaka 2014 baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyowakilishwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Serikali ya Falme ya Oman iliyowakilishwa na Ofisi ya Diwan of Royal Cort ambapo ujenzi umefanywa na Kampuni ya Esteem Construction ya Dar-es-Salaam na kusimamiwa na Wahandisi wa Ofisi ya Diwan of Royal Cort ya Oman.

Msikiti huo mkubwa una nafasi ya kusaliwa na Waislamu zaidi ya 4,000 na una sehemu ya kusali wanaume na wanawake, vyumba sita vya madarasa, maktaba, maabara ya lugha na kompyuta, ukumbi wa mihadhara ya shughuli za kidini pamoja na maegesho ya gari.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo msikiti huo wa kisasa ambao unatarajiwa kuendesha ibada na pia kutoa mafunzo mbali mbali ya Dini ya Kiislamu na lugha mbali mbali ikiwemo lugha ya kiarabu.

Mapema Mwakilishi wa Serikali ya Oman na Katibu Mkuu wa Kituo Kikuu cha Sayansi na Utamaduni cha Sultan Qaboos, Habib bin Mohammed Al Riyami alisema kuwa ujenzi wa msikiti huo ni njia moya wapo ya kujenga uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Zanzibar na Oman na kuahidi kuwa Oman chini ya uongozi wa Mfalme Qaboos itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza sekta za maendeleo ikiwemo elimu pamoja na kuiimarisha dini ya Kiislamu.

Mufti Mkuu wa Zanzibar Saleh Omar Kabi alieleza fadhila za kujenga msikiti pamoja na kuendeleza elimu ya dini ya Kiislamu na kusisitiza kuwa wananchi wa Oman wakiongozwa na Sultan Qaboos wameendelea kuonesha udugu wa damu kati yao na wananchi wa Zanzibar kama ilivyokuwa kwa Aus na Hazraj wakati wa Mtume Mohammad (SAW).

Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Oman, Masheikh pamoja na wananchi walihudhuria katika ufunguzi wa msikiti huo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Balozi Mdogo wa Oman Dk. Ahmed Hamoud Al Habsi na viongozi wengineo.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...