SERIKALI imewataka wananchi kuunga mkono juhudi za usafi kwa kunawa mikono na sabuni ili kujikinga na maradhi yatokanayo na uchafu ili kujenga Taifa lenye watu wenye afya bora.

Akizungumza katika kilele cha wiki ya unawaji mikono kwa maji na sabuni iliyofanyika Kata ya Kiwalani, Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Ubora wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam(DAWASA), Dk Sufiani Masasi alisema kama Taifa ni muhimu kuwekeza nguvu katika kuelimisha jamii hasa umuhimu wa kunawa mikono na majisafi na sabuni ili kujenga Taifa lenye afya bora.

Akizungumza na jumuiya ya wananchi, waalimu na wanafunzi wa shule za msingi Umoja, Yombo, Mwale na Bwawani, Dk Masasi alisema DAWASA ni mdau muhimu wa usafi wa mazingira ndio sababu waliamua kuadhimisha wiki hiyo kwa kutoa elimu kwa walimu 44 kutoka katika shule hizo pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ya mtaa ili wawe mabalozi
wazuri katika kuwaelimisha wanafunzi juu ya umuhimu wake.

Alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni ‘Mikono safi kwa manufaa ya sasa na baadae’ inaikumbusha jamii kuona umuhimu wa kunawa mikono na sabuni ili kujikinga na maradhi yatokanayo na uchafu.

Hivyo alitaka juhudi za pamoja zichukuliwe kuhakikisha wanafunzi wanaelewa umuhimu wa kunawa mikono kwani wao ndio wazazi wa siku zijazo na kwamba DAWASA itaendelea kuunga mkono kampeni za usafi hasa kwa kuendelea kubuni na kutengeneza miundombinu ya majisafi katika Maeneo mbalimbali ya jiji.

Dk Masasi alisema tayari DAWASA imefanikiwa kufikisha mradi huo wa majisafi kwa shule hizo ambapo utanufaisha wanafunzi 5123 pamoja na zahanati ya eneo hilo na kwamba itaendelea kufadhili miradi ya aina hii ili kuunga mkono juhudi hizo za usafi wa mazingira.

Mkufunzi wa mafunzo kwa walimu wa shule hizo, Juhudi Nyambuka ambaye ni Afisa Afya Manispaa ya Temeke alipongeza juhudi za DAWASA katika kusaidia jamii kupata huduma za majisafi na kueleza zitasaidia kupunguza magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji.

Katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma rasmi za maji ya bomba DAWASA, jumuiya za wananchi pamoja na wadau wa maendeleo wamekuwa wakijenga miradi ya maji kupitia programu ya maji na usafi wa mazingira kwa jamii. 

Miradi hiyo ipo katika maeneo mbalimbali kama vile Ukonga, Yombo, Kitunda, Mbagala, Kijichi, Feri,Kigamboni.Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha.
Wanafunzi wa Shule za Msingi zilizopo Kata ya Kiwalani wakishiriki igizo lenye lengo la kuelimisha jamii umuhimu wa kunawa mikono na majisafi na sabuni wakati wa kilele cha wiki ya unawaji mikono kwa maji na sabuni yaliyofanyika Kiwalani Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...