Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo ambaye pia ni mlezi wa TPF NET mkoa wa Arusha akikabidhi Mbuzi wawili pamoja na zawadi mbalimbali zenye thamani ya Shilingi 780,000 na fedha taslimu Shilingi 160,000/= kwa watoto yatima wa kituo cha Christ Hope Orphonage kilichopo jijini hapa.
 Wanachama wa Mtandao wa Polisi Wanawake Arusha pamoja na watoto yatima wa kituo cha Christ Hope Orphonage wakionekana kusikiliza kwa umakini hotuba iliyokuwa inatolewa na mlezi wa Mtandao huo Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo.
Askari wapatao 80 toka wilaya mbalimbali za mkoa wa Arusha ambao ni wanachama wakitembea kwa maandamano umbali wa kilomita 7 huku wakiongozwa na Brass Band ya Polisi. 
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
MTANDAO wa Polisi Wanawake mkoa wa Arusha umetakiwa upambane kwa kujitoa na kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu ili kuweza kutokomeza ndoa za utotoni kwa baadhi ya makabila.

Hayo yameelezwa leo na mlezi wa mtandao huo mkoani hapa ambaye pia ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu kamishna (DCP) Charles Mkumbo wakati wa maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwa mtandao huo yaliyolifanyika katika kituo cha kulelea watoto yatima kiitwacho CHRIST HOPE ORPHANAGE kilichopo Uswahilini halmashauri ya jiji la Arusha.

Aliwataka wasimame imara ili kuhakikisha elimu juu ya unyanyasaji na ukatili kwa watoto, akina mama na akina baba inatolewa na kuwafikia walipo hali ambayo itasaidia kuondoa kabisa tatizo hilo.

Kamanda Mkumbo alisema wakati umefika sasa kwa Madawati ya Jinsia na watoto kutokaa ofisini na badala yake wanatakiwa waifuate jamii ilipo kwani wanaokwenda kutoa taarifa kwenye vituo vya Polisi ni sehemu ndogo tu ya wengi wenye kukosa elimu ya uelewa juu ya ukatili na unyanyasaji waliopo mitaani.

“Wale wanaokwenda kutoa malalamiko yao katika vituo vya Polisi ni wachache sana ukilinganisha na wale wenye matatizo hayo waliopo mitaani au kwenye taasisi mbalimbali kama vile shule” Alisema kamanda Mkumbo.

“Watu wengine mpaka leo hii wanaamini ukeketaji ni moja ya mila yao kitu ambacho sio sahihi hivyo kupitia madawati ya Jinsia na Watoto pamoja na taasisi nyingine zikishirikiana na kutembelea jamii kwa nia ya kuwaelimisha naamini kwamba matatizo haya yataisha”. Aliongeza Kamanda Mkumbo.

Aliwatake wanachama wa mtandao huo ambao ni Polisi Wanawake kufanya kazi kwa bidii ili kuidhihirishia jamii kwamba wanaweza bila kuwezeshwa. Alimalizia Kamanda Mkumbo.

Awali akieleza madhumuni ya maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi  Namsemba Mwakatobe, alisema kwamba mtandao huo una wajibu wa kushirikiana na na makundi mbalimbali wakiwemo watoto yatima hali ambayo itasaidia makundi hayo kutambua kwamba, hawapo peke yao bali mtandao huo upo nyuma yao katika kusikiliza matatizo yao na kulinda haki zao.

Alisema pamoja na kuungana nao siku ya leo lakini pia mtandao huo umejitokeza  kwa ajili ya kuonyesha upendo wao kwao kama askari lakini pia kama wa kike na kuhakikisha kwamba wanakuwa katika mazingira salama na kuepuka vitendo vya uhalifu.

Akizungumza katika maadhimisha hayo Mkurugenzi wa kituo hicho Bw. Steven Isanja alisema kituo hicho kilianzishwa mwaka 2007 kikiwa na watoto 30 lakini hivi sasa kina watoto 64 ambao wanasoma katika ngazi ya Chekechea, Shule ya Msingi na Sekondari.

Maadhimisho hayo yaliyojumuisha jumla ya askari wanawake 80  kutoka wilaya za mkoa huu yalianzia katika kituo kikuu cha Polisi Arusha ambapo walitembea kwa maandamano umbali wa kilomita 7 kisha kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wa kituo hicho kama vile Mchele kilo 100, Mbuzi wawili, mafuta lita 40, sabuni  vinywaji mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya Shilingi 780,000/= pamoja na fedha taslimu shilingi 160,000/=.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...