SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imesema itaendelea kukijengea uwezo Chuo cha Usimamizi wa Kodi Nchini (ITA) ili kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinazalisha Wataalamu  bora wenye kukithi  mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila wakati wa mahafali ya kumi cha Chuo cha Kodi Nchini (ITA) na kuongeza kuwa malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinazalisha wataalamu wenye umahiri katika masuala ya forodha na kodi.
Dkt. Kayandabila alisema Serikali inatambua umuhimu wa Chuo hicho kwa ustawi wa kiuchumi na kijamii, hivyo kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaendelea kukipangia Chuo hicho bajeti ya maendeleo ili kukithi matumizi yake ya kimaendeleo ikiwemo kufanya tafiti kwa kiwango kinachohitajika.
“Serikali itaendelea kushirikiana na Chuo cha Kodi kupitia Mamlaka ya Mapato kwa kuhakikisha kuwa mipango yenu hususani Mpango Mkakati wa Nne unaoanza kutekelezwa mwaka 2017/18 unatekelezwa kikamilifu kwa kuwapatia hosteli mpya za wanafunzi, upanuzi wa majengo ya ofisi za wakufunzi na ujenzi wa kampasi mpya ya Misugusugu Kibaha Mkoani Pwani” alisema Dkt. Kayandabila.
Dkt. Yamungu aliwataka wahitimu hao kutambua kuwa Serikali inatambua umuhimu na mahitaji ya Wataalamu wa kodi, hivyo Chuo hicho hakina budi kuzalisha wataalamu watakaosaidia juhudi za Serikali za kukuza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi kwa wafadhili.
Aliongeza kuwa pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na Chuo hicho, Dkt. Kayandabuila aliutaka Uongozi wa Chuo hicho kuendelea kujiimarisha katika utafiti na kutoa mafunzo katika masuala ya kodi hususani sekta ya uchimbaji madini, mafuta na gesi na sekta ya fedha ili kusaidia kuongeza makusanyo ya mapato katika sekta hizo. 
Akifafanua zaidi Kayandabila alisema utafiti katika sekta za madini, mafuta na gesi utasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kukuza mapato ya ndani na kuongeza uwezo wa Serikali kutoa huduma za kijamii na kusimamia viwanda.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kicheere alisema Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinazalisha Wataalamu bora wa forodha na kodi pamoja na kupanua wigo wa ushirikiano na mataifa ya nje ikiwemo Botswana, Kenya, Burundi na Sudan Kusini.
Alisema kupitia Chuo hicho mamlaka yake imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inaweza kuzalisha wataalamu wake wa ndani na kupunguza gharama ya kuchukua wataalamu wa nje ya nchi kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya forodha na kodi.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa ITA kinazalisha wataalamu bora sambamba na kuendelea kuwa  kuwa na Chuo cha Umahiri kama tulivyopendekezwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki” alisema Kicheere.   
Naye Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Isaya Jairo alisema tangu Chuo kilipopata usajili kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) wameweza kutoa kudahili wanafunzi 6000, ambapo ili kupanua wigo wa masomo ya forodha na kodi, Chuo hicho kimepanga kushirikiana na vyuo mbalimbali vya nje ya nchi.
Aliongeza kuwa pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana hadi sasa, Chuo hicho kinaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wanafunzi wengi wa masomo ya shahada kushindwa kuhitimu masomo yao kutokana na ukosefu wa ada.
 Baadhi ya Wanafunzi  wa Chuo cha Usimamizi wa Kodi  (ITA) pichani wakifuatilia hotuba zilizokuwa zikitolewa na wageni mbalimbali waliohudhuria mahafahali ya 10 ya Chuo hicho yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Novemba 11, 2017. 
 Baadhi ya ndugu na jamaa za wanafunzi waliohitimu katika Chuo cha Usimamizi wa Kodi wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa mahafali ya 10 ya Chuo hicho yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Novemba 18, 2017.
 Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa Malamka ya Kodi Tanzania (TRA), (katikati) Richard Kayombo akijadiliana jambo na Maafisa Waandamizi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) wakati wa  mahafali ya 10 ya Chuo hicho yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Novemba 18, 2017.
 Viongozi na Wahadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Kodi wakiongozwa na kikosi cha bendi cha Jeshi la Polisi kuingia katika ukumbi wa Multipurpose katika Chuo hicho wakiwa tayari kuanza mahafali ya 10 ya Chuo hicho yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Novemba 18, 2017.

Viongozi na Wahadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Kodi wakiongozwa na kikosi cha bendi cha Jeshi la Polisi kuingia katika ukumbi wa Multipurpose katika Chuo hicho wakiwa tayari kuanza mahafali ya 10 ya Chuo hicho yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Novemba 18, 2017.
Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 10 ya Chuo cha Usimamizi wa Kodi (ITA), Dkt. Yamungu Kayandabila (kushoto) akiongozwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kicheere kuingia ukumbini kwa ajili ya kuanza kwa hafla ya mahafali ya 10 ya Chuo hicho yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Novemba 18, 2017.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...