Kaimu Katibu Tawala mkoa Mara Bw. Raphael Nyanda akifungua mkutano wa Wadau wa Huduma za Ustawi wa Jamii katika mkoa wa Mara kupata maoni kuhusu Utafiti wa Mfumo wa Kisheria wa Huduma za Ustawi wa Jamii nchini. Utafiti huo unaendeshwa na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.
Mmoja wa Wdau wa mkoa wa Mara Mwl. Masumbuko Marco akichangia maoni wakati wa Utafiti kuhusu Mfumo wa kisheria wa Huduma za Ustawi wa Jamii Tanzania.
Wadau wakichangia maoni katika mkutano wa Utafiti kuhusu mfumo wa kisheria za Huduma za Ustawi wa Jamii mkoani Mara.

Na Munir Shemweta, TUMESHERIA

Serikali mkoa wa Mara imewataka wadau wa sekta ya huduma za ustawi wa jamii kuangalia namna sheria zinavyotekelezwa badala ya kujikita katika kuangalia sheria pekee ambazo wakati mwingine hazina tatizo. Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara Raphael Nyanda wakati akifungua kikao cha wadau wa mkoa wa Mara wakati wa Utafiti wa Mfumo wa Kisheria wa Huduma za Ustawi wa Jamii Tanzania. Utafiti huo unaendeshwa na Tume ya Kurekebisha Sheria katika mikoa mbalimbali ya Tanzania bara.

Alisema, inawezekana wakati mwingine sheria iliyopo ni nzuri lakini tatizo linakuwa ni mifumo migumu inayosababishwa na watu wanaosimamia ama kutekeleza sheria hiyo. ‘’ cha msingi wakati wa kuangalia sheria zinazohusiana na masuala ya ustawi wa jamii wadau wanapaswa kuangalia pia namna sheria zinavyotekelezwa badala ya kuangalia sheria husika pekee’’ alisema Bw. Nyanda. Kaimu Katibu Tawala huyo wa mkoa wa Mara, alisema makundi mengine kama mila, desturi na tabia navyo vinaweza kupelekea uharibifu wa sheria zetu hivyo amewataka wadau wasijikite katika sheria na badala yake waangalia masuala mengine yanayoendana na sheria husika.

Ameshauri vikao vya wadau kupitia sekta ya huduma za ustawi wa jamii vihusishe pia watu ambao hawapo moja kwa moja katika sekta hiyo kwani wanaweza kuchangia mambo ya msingi na hivyo kuifanya Tume kuja na mapendekezo ambayo mwisho wa siku yatakuja na matokeo chanya. Amewataka washiriki wa mkutano huo kusoma na kuzielewa vizuri sheria za masuala ya ustawi wa jamii sambamba na kuangalia maeneo yote yenye matatizo na kuyatolea maoni yatakayoleta tija katika mfumo mzima wa huduma za ustawi wa jamii.

Aidha, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara aligusia matatizo ya huduma za ustawi wa jamii katika mkoa wake kuwa ni unyanyasaji wa wazee na akina mama, masuala ya ardhi ambapo alitolea mfano wilaya ya Rorya kuwa ni moja ya maeneo yanayoongoza kwa matatizo hayo katika mkoa wake. Kwa upande wake katibu Msaidizi wa Tume ya Kurekebisha Bi. Agnes Mgeyekwa alisema kwa sasa Tume inafanya Utafiti kuhususiana na Huduma za Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto lengo likiwa kuja na mapendekezo yatakayosaidia uanzishwaji wa sheria ama kuboreshwa kwa maeneo mbalimbali katika sekta ya huduma za ustawi wa jamii.

Kwa mujibu wa Mgeyekwa mbali na kutembelea mkoa wa Mara katika Utafiti huo pia Tume ilitembelea mikoa ya Kigoma, Kagera, Njombe, Rukwa, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Tabora na Mtwara na kubainisha kuwa lengo likiwa ni kupata maoni ya wadau wengi katika mikoa tofauti hasa ikizingatiwa huduma za ustawi wa jamii zimekuwa zikiathiri maisha ya watu, makundi ya watu na hivyo kusababisha umasikini, kusambaratika kwa familia, kuvunjika kwa ndoa, huduma mbovu za afya na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...