WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa mwezi mmoja Ofisa Ardhi wa wilaya ya Namtumbo Bw. Maurus Yera awe ametafuta ardhi ya kuwafidia wakazi wa kijiji cha Lwinga wilayani Namtumbo. Wakazi hao 21 mwaka 2008 eneo lao lenye ukubwa wa ekari 101 lilitwaliwa na Serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupisha ujenzi wa shule ya sekondari ya mkoa wa Ruvuma na waliahidiwa kulipwa fidia.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Novemba 23, 2017) alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Lwinga akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma. Alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi hao kupitia mabango, ambapo walimuomba awatatulie kero hiyo ya madai ya fidia ya ardhi iliyodumu kwa miaka 10 bila kupatiwa ufumbuzi.

Waziri Mkuu alisema haoni sababu ya Halmashauri hiyo kushindwa kuwafidia wananchi hao sehemu ya ardhi kwa muda wote huo ukizingatia wilaya hiyo ina hifadhi ya ardhi. 
“Nataka wananchi hawa wawe wamelipwa fidia yao ya ardhi kabla ya siku kuu ya Krismasi ya mwaka huu. Serikali haiko tayari kuona wananchi wake waliotoa ardhi kupisha maendeleo wakisumbuliwa," alisema Waziri Mkuu na kuongezea kwamba Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inataka kila mtumishi ahakikishe anatumia taaluma yake vizuri kwa kuwahudumia wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili kwa wakati.

Pia Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi hao kuhakikisha hawakubali kutoa rushwa pale wanapohitaji kupata huduma mbalimbali kutoka kwa watumishi kwa kuwa ni haki yao kuhudumiwa.Aliwataka wananchi kuwa na imani na Serikali yao na kuiunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa kwani vitendo hivyo vinakwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...