NA. Estom Sanga- Tanga

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe. George Huruma Mkuchika amewaagiza viongozi wa halmashauri za wilaya nchini kote kusimamia kwa karibu utekelezwaji wa miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF- ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Akizungumza mwanzoni mwa ziara yake ya kukutana na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- katika jiji la Tanga Waziri Mkuchika amesema ufanisi wa Mpango huo umeanza kuonekana kutokana na idadi kubwa ya Walengwa kuanza kuboresha maisha yao hivyo kinachotakiwa ni kuweko na dhamira thabiti ya wataalamu hususani wa Maendeleo ya Jamii ambao wanaweza kutoa mchango muhimu zaidi kwa Walengwa.

Mheshimiwa Mkuchuka amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi hususani wanaokabiliwa na umaskini ili waweze kuondokana na kadhia hiyo kupitia mipango mbalimbali ukiwemo Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF.

Aidha Mhe. Mkuchika ameonya dhidi ya uwezekano wowote wa kuhudumia wananchi wenye uwezo katika Mpango huo na kuagiza Watendaji wa halimashauri za Wilaya kuhakiki mara kwa mara majina ya kaya zilizoko kwenye Mpango ili kujiridhisha na walengwa wa Mpango ambao ni kaya Maskini sana.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuchika ametembelea kaya za baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini katika jiji la Tanga na kujionea namna ruzuku wanaoipata ilivyoanza kuboresha maisha yao kwa kuboresha makazi ,kuanzisha miradi midogo midogo ya biashara, kusomesha watoto na kuimarisha huduma za kliniki kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Taarifa ya Mkoa wa Tanga imeonyesha kuwa tangu shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini zianza takribani miaka mitatu iliyopita Kaya zilizokuwa zinaishi katika umaskini mkubwa wa kipato zimeanza kuboresha maisha huku changamoto kubwa iliyobakia ikiwa ni idadi nyingine ya wananchi wanaoishi kwenye Umaskini mkubwa wa kipato kutojumuishwa kwenye mpango kutokana na uhaba wa fedha. 
 Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma  na Utawala Bora,Mhe. George Huruma Mkuchika (aliyevaa Kaunda suti )akiangalia ‘genge’ la bidhaa zinazouzwa na mmoja wa Walengwa wa TASAF katika mmoja wa mtaa wa jiji la Tanga.

 Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Huruma Mkuchika akimpongeza mmoja wa Walengwa wa TASAF jijini Tanga baada ya kukagua nyumba aliyoijengwa kwa kutumia sehemu ya ruzuku ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini .
 Baadhi ya Viongozi walioambatana na Mhe. Mkuchika (wa nne kulia walioketi) wakisikiliza taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF katika mmoja wa mitaa ya jiji la Tanga. Wa pili kulia waliosimama ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,bwana Ladislaus Mwamanga. 
 Waziri Mkuchika akiwa ameketi nje ya mgahawa wa mmoja wa Walengwa TASAF katika jiji la Tanga ,Mgahawa ambao ameuanzisha mlengwa huyo baada ya kupata ruzuku kutoka Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato. 
 Mhe. Mkuchika akiwa ndani ya nyumba ya mmoja wa Walengwa wa TASAF ,katika jiji la Tanga ,nyumba ya mlengwa huyo imeezekwa kwa mabati kwa kutumia sehemu ya ruzuku kutoka Serikalini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Huruma Mkuchika akizungumza na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Tanga na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga kabla ya kuwatembelea walengwa wa TASAF kuona namna wanavyonufaika na huduma za Mfuko huo mkoani humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...