Serikali imewataka wanufaika wa ruzuku ambao hawakuitumia kama
ilivyokusudiwa warejeshe fedha walizopatiwa mara moja na vyombo vya
ulinzi na usalama vihakikishe waliohusika kuidhinisha wanawajibishwa.
Agizo hilo limetolewa Desemba, 12, 2017 na Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo Mkoani Singida wakati wa ziara yake ya kutembelea
Migodi ya Dhahabu kwa ajili ya kujionea shughuli zinazoendelea na
kuzungumza na wachimbaji.
“Aliyenufaika na ruzuku na hakufanya lolote, arejeshe mara moja fedha
hiyo na aliyehusika kuwapatia ruzuku watu hawa hali yakuwa anaelewa
hawakuwa na dhamira ya kuendeleza uchimbaji nae achukuliwe hatua,”
aliagiza Nyongo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto aliyenyoosha
mkono) akielekeza jambo alipotembelea Mgodi wa Dhahabu wa
Mwandami Small Scale Mine uliopo katika Kijiji cha Sambaru, Kata ya
Mang’onyi Wilayani Ikungi.
Agizo hilo linafuatia malalamiko ya wachimbaji wadogo ambao
hawakunufaika na mpango huo wa ruzuku ambapo walimueleza
kwamba wapo baadhi ya watu wasiostahili lakini walipatiwa ruzuku.
Naibu Waziri Nyongo alisema anampongeza Rais John Magufuli kwa
uamuzi wake wa kusimamisha utoaji wa ruzuku kwani imeshindwa
kufikia matarajio yaliyokusudiwa.
Alisema Serikali ilisimamisha utoaji wa ruzuku kwa wachimbaji wadogo
wa madini nchini baada ya kubaini kwamba imeshindwa kuleta
mafanikio yaliyokusudiwa.
Nyongo alisema dhamira ya Serikali ya kutoa ruzuku ilikuwa ni
kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini nchini wanaweza
kuendeleza machimbo yao kwa kufanya shughuli zenye tija kwao na
Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo alisema dhamira hiyo haikuzaa matunda yaliyokuwa
yamekusudiwa kwani imedhihirika kwamba ruzuku iliyotolewa
haikuwanufaisha walengwa kama ilivyotarajiwa badala yake ilinufaisha
watu wachache tofauti na ulivyokuwa mpango mzima wa utoaji wake.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akitazama
mtambo wa kusaga mawe yenye Madini ya Dhahabu uliopo kwenye
Mgodi wa Mzaki na Wenzake uliopo katika Kijiji cha Mwau, Wilayani
Ikungi. Kulia ni Mmoja wa Wamiliki wa mgodi huo, Kasirate Mzaki.
“Wapo wachimbaji wachache ambao walifanikiwa kupata ruzuku na
waliweza kuendeleza migodi; japo hawa ni wachache tofauti na malengo
ya Serikali,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Mbali na hilo, alisema baadhi ya wachimbaji wadogo walipewa ruzuku
na walichimba lakini hawakufanikiwa kwani walichimba kwa kubahatisha
bila kuwa na elimu ya kutosha ya kutambua uwepo wa mashapo katika
maeneo yao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...