Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa miezi mitatu kwa wananchi wanaoishi katika kambi ya uvuvi ya Nankanga iliyopo kando ya ziwa Rukwa kuhama kwa hiyari baada ya kambi hiyo kuwa katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kipindupindu kwa kutokuwa na vyoo.

Mh. Wangabo amesema kuwa kuondoka huko kwa hiari kuwepo ndani ya mwezi huu wa kwanza hadi wa nne baada ya kuona wingi wa wananchi wanaoishi katika kambi hiyo pamoja na kutokuwepo kwa kipindupindu kwa wakati huu ila zoezi hilo ni la tahadhari ili kujikinga na ugonjwa huo.

“Hatuwezi kuendelea kuishi mahali hapa ambapo vyoo vyenyewe vinaingiliana na maji ya kunywa, na ili kisije hapa kipindupindu ni lazima watu wasifanye shughuli kwenye ziwa ili kuwe salama, lakini mkiruhusu kipindupindu kuingia hapa tutawafurusha, tena tutawasimamia kweli kweli, tutawapiga quarantine (kuwaweka kwenye kizuizi) mkipona tutawaswaga,” Amesisitiza

Ameyasema hayo alipofanya ziara kwenye kambi ya Nankanga iliyopo katika Kijiji cha Solola Wilayani Sumbawanga ili kujionea hali halisi ya maisha ya wavuvi katika kambi zisizo rasmi na namna ya kuweka mpango salama wa kuweza kuwaepusha na ugonjwa wa kipindupindu ulioenea katika makambi hayo yanayozunguka ziwa Rukwa. 

Nae Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule alitoa hadi tarehe 1/5/2018 wananchi hao wawe wameyahama makazi hayo na kujisogeza kwenye vitongoji vya jirani huku akiwasihi viongozi wa vijiji na vitongoji hivyo kushirikiana kuhakikisha wanatoa maeneo kwaajili ya wananchi hao kuhamia.

“Kuanzia tarehe 1 mwezi wa 5 hapa hatutaki kumuona mtu, kama una kibanda chako ama bati lako anza sasa hivi kwa kushirikiana na mwenyekiti wa Kijiji na Mtendaji wa Kata mtafute nafasi katika kitongoji cha Isanga kila mtu ajenge nyumba,” Alisisitiza.

Hatua hiyo imekuja baada ya ugonjwa wa kipindupindu kusambaa kwenye kambi kadhaa za wavuvi pembezoni mwa ziwa rukwa na kusababisha watu 210 kuumwa ugonjwa huo na watu nane kupoteza maisha, ambapo hadi sasa kambi zisizo rasmi zaidi ya tisa zimefungwa huku zoezi hilo likitegemewa kuendelea hadi hapo Mwezi wa tano.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa kwanza mbele kulia) akiwa ameambatana na mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule wakitembelea kambi ya mererani waliyohamishwa wavuvi kwa nguvu ili kuepuka kipindupindu na kulinda mazingira ya ziwa hilo. 
 Moja ya kibanda kilichokuwa katika kambi ya Wavuvi ya Mererani kikiwaka moto ikiwa ni juhudi za kuwaondoa wavuvi waliopo ndani ya Ziwa Rukwa kuwaepusha na kipindupindu na kulinda ziwa lisipotee. 
 Miongoni mwa wananchi waliokuwa wakiishi katika makambi ya wavuvi yalipo ndani ya Ziwa Rukwa yaliyoathiriwa na kipindupindu wakisimamiwa kuhama kambi hiyo ili kujiepusha na kipindupindu na kuliza Ziwa.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa tahadhari kwa Wavuvi waliohamishwa kwenye makambi (hawapo pichani) kutorudi katika makambi hayo kwa usalama wa afya zao na kuendelea kulitunza ziwa Rukwa. 
 Miongoni mwa Vyoo vinavyotumiwa na Wavuvi wa kambi ya Nankanga waliopewa miezi mitatu kuihama kambi hiyo kabla ya kipindupindu kuwamaliza. 
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipoongozana na kamati ya ulinzi na Usalama kuangalia moja ya choo kinachotumiwa na wavuvi wa kambi ya Nankanga, choo ambacho si salama kwa matumizi ya binadamu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...