Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, ambayo haina hospitali ya Wilaya imejipanga huhakikisha inaanza mchakato wa ujenzi wa hospitali hiyo. 

Wilaya ya Simanjiro iliyoanzishwa mwaka 1993 baada ya kugawanywa kutoka wilaya ya Kiteto, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 ina wananchi 178,693 lakini hadi hivi sasa haina hospitali ya wilaya. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Yefred Myenzi aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo. 

Myenzi alisema viongozi na wananchi wa wilaya hiyo kwa pamoja wanapaswa kushikamana ili kuhakikisha wanafanikisha ujenzi wa hospitali hiyo ya wilayani. 
Alisema ameshakutana na wataalamu wa idara ya afya waliotoka ofisi ya Rais Tamisemi, waliofika ofisini kwake na kupanga mipango ya kuanzisha hospitali ya wilaya hiyo. 

"Sikubaliani na pendekezo la kukipandisha hadhi kituo cha afya Orkesumet ili kiwe hospitali ya wilaya, hapana tunapaswa kujenga hospitali ya wilaya na kituo cha afya Orkesumet kitaendelea kufanya kazi yake kama kawaida," alisema Myenzi. 
Alisema tangu wilaya hiyo ya Simanjiro ianzishwe haijawahi kuwa na hospitali ya wilaya, hivyo huu ni wakati muafaka wa kuanza mchakato wa ujenzi wake. 

Diwani wa Kata ya Orkesumet, Sendeu Laizer alisema anaunga mkono hatua ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Yefred Myenzi kuanza ujenzi wa hospitali mpya ya Wilaya na kutopandisha hadhi kituo cha afya cha Orkesumet. 
Laizer alisema suala hilo ni maendeleo makubwa kwa wananchi wa kata ya Orkesumet na Wilaya ya Simanjiro kwa ujumla kwani wilaya hiyo haijawahi kuwa na hospitali ya wilaya tangu ianzishwe. 

Mkazi wa wilaya hiyo Meshack Tureto alisema ujenzi wa hospitali hiyo, itakuwa ni maendeleo mazuri kwa wananchi wa eneo hilo, ambao hawana hospitali ya wilaya. 
Tureto alisema uanzishwaji wa hospitali ya wilaya itakuwa ni muendelezo mzuri wa maendeleo kwenye eneo la afya, kwani mgonjwa ataweza kupata rufaa ya ugonjwa kwa ukaribu zaidi tofauti. 

Mkazi wa Orkesumet, Baraka John alipongeza jitihada za Myenzi kuanzisha mchakato wa ujenzi wa hospitali hiyo kwani anaamini mikakati hiyo itafanikiwa. 
"Tunaposema uongozi wa ubunifu na unaoacha alama ni huu alioufanya mashine ya kazi Myenzi kwani hospitali ya wilaya ni hitaji la muda mrefu kwa jamii ya eneo hili," alisema John.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara Yefred Myenzi akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Albert Msole na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Zuwena Omary. 
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Albert Msole akizungumza wakati akifungua kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo, kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Zuwena Omary na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Yefred Myenzi.  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...