Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii.

Mkurugenzi wa Saha Limited  na mwingine wa Lucky Shipping Co.Ltd, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka mawili ya uhujumu uchumi ikiwemo kupeperusha bendera ya Tanzania bila kibali kwa nia ovu.
Mwendesha Wakili wa Serikali, Wankyo Saimon amewataja washtakiwa hao kuwa ni Issa Haji au Salum (39) ambaye ni baharia na Mkurugenzi wa Kampuni ya Lucky Shipping pamoja na Abdullah Hanga (73) mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Kampuni ya Saha ambaye ni mkazi wa Mbezi Beach.
Washitakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa uhalifu kinyume sheria inayohusiana na vyombo vya baharini na Sheria ya Uhujumu uchumi.

Akisoma hati ya mashtaka wakili Simon amedai katika tarehe tofauti tofauti, kati ya Julai 19, mwaka jana na Januari 16, mwaka huu jijini Dar es Salaam,washtakiwa hao, walitoa ushauri, msaada na maelekezo katika kutenda kosa la jinai la mtandao wa uhalifu.
Amedai, kosa hilo ni kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye meli iitwayo ‘Huihang 68’ ambayo zamani ilijulikana kama Greko 02, bila kuwa na hati ya usajili kutoka kwa msajili wa meli nchini kwa lengo la kujipatia faida kutoka katika shughuli za uvuvi haramu.
Pia imedaiwa kuwa Julai 19, mwaka jana na Januari 16, mwaka huu ndani ya jiji la Dar es Salaam washitakiwa hao huku wakifahamu kuwa ni kosa kisheria waliruhusu upeperushwaji wa bendera katika meli hiyo bila kuwa na leseni kutoka kwa msajili wa meli kwa lengo la kuifanya ionekane kuwa ya Tanzania wakati sio kweli.
Hata hivyo, washitakiwa hawakutakiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.Hata hivyo, Saimon alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuieleza mahakama taarifa za upelelezi huo umefikia wapi.
Aidha upande wa mashtaka ulidai Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa washitakiwa hao kwani wakipewa dhamana wataingilia maslahi ya Taifa hivyo mahakama ijielekeze katika suala hilo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 22, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na upande wa utetezi kuwasilisha hoja zao kuhusu mapingamizi ya  hati ya DPP washitakiwa wamerudishwa rumande.
Watuhumiwa ambao ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Lucky Shipping,   Issa Haji au Salum(kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Saha, Abdullah Hanga (Kushoto)  wanaodaiwa kujihusisha na uhujumu uchumi ikiwemo kupeperusha bendera ya Tanzania bila kibali kwa nia ovu wakiwa mahakamani wakisubiri kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...