WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaasa wanaume wa wilaya ya Tarime kujiepusha na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kuachana na kilimo cha bangi.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatano, Januari 17, 2018) wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Serengeti, wilayani Tarime.

Waziri Mkuu alisema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kilimo cha bangi vinaitia doa wilaya hiyo, hivyo hawana budi wakaepukana navyo.

“Serikali inakemea vitendo vya ukatili, achaneni navyo. Mtu unamchapa mtoto makofi hadi anazimia, kitendo hicho hakiwezi kuvumilika na pia kinaitia doa wilaya yenu.”

Wakati Huo huo, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Glorious Luoga kuendelea na msako wa mashamba ya bangi na mirungi na kuchukua hatua kwa watakaobainika kuendesha kilimo hicho.

Alisema ardhi ya wilaya hiyo ni nzuri na inahimili kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara kama mahindi, mihogo, ndizi, kahawa, pamba, ni marufuku kulima bangi.

Pia Waziri Mkuu aliagiza kuchukuliwa hatua kwa wakandarasi waliotekeleza ujenzi wa maji mkoani Mara kwa sababu miradi hiyo wameijenga chini ya kiwango.

Waziri Mkuu aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kupitia mabango wakidai kutonufaika na miradi ya maji katika maeneo yao licha ya Serikali kutoa fedha.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, JANUARI 18, 2018.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...